1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mabingwa Ulaya:Gomez kuongoza mashambulizi ya Bayern

Aboubakary Jumaa Liongo19 Oktoba 2010

Majogoo 16 wa kandanda barani Ulaya wanaingia dimbani leo hii katika patashika ya kuwania ubingwa wa vilabu barani humo.

https://p.dw.com/p/Phqr
Mshambuliaji wa Bayern Munich Mario Gomez,Picha: picture alliance/dpa

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich waliyoko katika kundi E wako nyumbani kuwaalika CFR Cluj, huku Basel ikisafiri hadi Roma Italia kupambana na AS Roma.

Roma itamtegemea sana mshambuliaji wake mkongwe Francesco Totti ambaye kocha wa timu hiyo Ranieri amesema kiwango chake kimepanda sana.

Kwa upande wa pambano la Bayern na CFR, mabingwa hao wa Ujerumani wanaokabiliwa na balaa la majeruhi wengi, watamtegemea mshambuliaji ghali wa timu hiyo Mario Gomez kuchomoza tena baada ya kupachika mabao matatu peke yake katika mechi ya Bundesliga mwishoni mwa wiki.

Gomez ambaye katika kikosi cha kwanza cha kocha wa Bayern Lois van Gaal hana nafasi, ameutumia mwanya wa kuumia kwa wachezaji wengi kuonesha makucha yake.Pia Bastian Schweinsteiger atakuwa uwanjani kuimarisha kiungo baada ya kupona majeraha yake.

Chelsea - Barcelona 1:0 Michael Essien
Mghana Michael Essien wa ChelseaPicha: AP

Katika Kundi F, Chelsea imerejea katika uwanja wa Luzhniki mjini Moscow ambao miaka miwili iliyopita mbele ya washabiki elfu 80 ilinyang´anywa tonge mdomoni na Manchester United katika fainali ya michuano hiyo.Chelsea inapambana na Spartak Moscow.

Katika fainali hiyo ya mwaka 2008, Chelsea iliondoshwa na Manchester United katika changamoto ya mikwaju ya penalti, ambapo nahodha wake, John Terry alikosa penalti muhimu kwa kuteleza wakati alipokuwa akijianda kupiga.

Mechi nyingine katika kundi hilo hii leo ni kati ya Olympique Marseille na Zilina.Lakini macho na masikio yanaelekezwa katika pambano la G katika Real Madrid na AC Milan, mjini Madrid.Madrid inajaribu kurejea tena katika kilele cha kabumbu barani Ulaya, huku jukumu akikabidhiwa Jose Mourinho.

Özil Coruna
Mesut Özil anayeangalia akishangilia moja ya mabao ya Real MadridPicha: picture-alliance/EXPA/Alterph

Madrid ina majogoo kadhaa akiwemo Sami Khedira na Mesut Ozil ambao ni viungo wakutegemwa wa Ujerumani, pamoja na Christiano Ronaldo.Mechi nyingine hii leo itakuwa ni kati ya Ajax Amsterdam na Auxerre, huku Arsenal wakiwa nyumbani jijini London kuwaalika dimbani Shakhtar Donetsk

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA/Reuters

Mhariri:Mohamed Abdulrahman