1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya Ujerumani yaingia duru ya nne; Arsenal yaoga mabao

Sekione Kitojo29 Agosti 2011

Bayern Munich yaongoza ligi ya Bundesliga, Schalke 04 ni ya pili, Manchester United yaipa kipigo cha mbwa mwizi Arsenal , Real Madrid yapata ushindi mnono katika ligi ya Hispania, Ujerumani yavuna medali ya kwanza

https://p.dw.com/p/12PTB
Wachezaji wa Bayern Munich wakifurahia bao dhidi ya Kaiserslautern katika bundesligaPicha: picture alliance/dpa

Tuanze na Bundesliga, ligi ya Ujerumani. Duru ya nne ya ligi ya Ujerumani Bundesliga , inaonyesha hata hivyo kuwa msimu bado ni mchanga, kutokana na hali ya mambo inavyokwenda. Lakini mabingwa mara nyingi wa Bundesliga Bayern Munich baada ya kufanya vibaya msimu uliopita, wameazimia kufanya kweli msimu huu. Wao sasa ndio vinara wa ligi, wakifutiwa na Schalke 04 na Werder Bremen. Licha ya msimu kuwa mchanga lakini , moja kati ya vigogo vya soka la Ujerumani , Hamburg SV wanaburura mkia katika msimamo wa ligi.

Mabingwa watetezi Borussia Dortmund wakipambana katika "Big Match" ya duru ya nne walipambana na makamu bingwa wa msimu uliopita Bayer Leverkusen na timu zote ziliridhika na sare ya bila kufungana katika mchezo ambao ulikuwa na hisia na jazba kubwa. Mlinzi wa mabingwa hao Borussia Dortmund Mats Hummels hata hivyo hakuridhika na matokeo hayo.

"Kuna awamu katika mchezo huo ambapo tumekuwa tukifanya vizuri, lakini pia kulikuwa na wakati tulipata matatizo kidogo. Lakini hilo halishangazi. Kwasababu Leverkusen hivi sasa wanacheza mchezo mzuri wa kushambulia. Na iwapo wanaongeza kasi, inakuwa si rahisi kuwazuwia. Na mbali ya hivyo , nadhani , Leverkusen walipata nafasi mbili za wazi, ambapo tuliwaruhusu kufanya hivyo. Hata hivyo ilikuwa sawa, lakini tungeweza pia kufanya vizuri zaidi".

Deutschland Fußball Bundesliga Borussia Dortmund gegen Eintracht Frankfurt
Fussball, 1. Bundesliga, Mlinzi wa kati wa mabingwa wa Ujerumani Borussia Dortmund Mats Hummels kuliaPicha: dapd

Hamburg SV baada ya kuangukia pua nyumbani dhidi ya FC Kolon imeporomoka na kushika mkia. Vigogo hao kutoka kaskazini mwa Ujerumani wamepata kipigo chao cha pili msimu huu kwa kuruhusu mabao 4-3 dhidi ya FC Kolon. Hali iliyoanza na matumaini kwa Hamburg iligeuka fadhaa baada ya kuachia ushindi dakika za mwisho , wakati ikiongoza kwa mabao 3-2. Waliiruhusu Kolon kusawazisha na katika dakika za majeruhi walipachika bao la 4 ambalo kwa kiasi kikubwa ni uzembe wa walinzi na mlinda mlango.

Mlinzi wa kushoto wa Hamburg Denns Aogo baada ya firimbi ya mwisho haikuwa rahisi kumtuliza.

"Siwezi kuamini, naweza kusema. Ilikuwa hali ya vuta nikuvute. Siwezi kuamini, ni kiasi gani tuliwajibika. Tumeona , jinsi kila mmoja alivyojitahidi. Na kisha kunatokea makosa kama yaliyotokea. Siwezi hata kuelezea. Kwa kweli naweza kusema sina maneno ya kuelezea".

Wakati Hamburg SV ikijikuta haina majibu, Schalke 04 ilikuwa inaelea angani, ikizuka katika nafasi ya 2 ya msimamo wa ligi baada ya Raul kuipatia bao pekee dhidi ya Borussia Moenchengladbach, timu ambayo msimu uliopita ilikuwa nusura ishuke daraja lakini msimu huu inakula sahani moja na vigogo wa ligi.

Kocha wa Schalke Ralf Rangnick anasema:

"Tumefarijika kutokana na maendeleo hayo, ambapo timu yetu hivi sasa inapata mafanikio. Leo nafikiri tumecheza vizuri kutokana na umiliki wa mpira wa wapinzani wetu. Kwa mtazamo wangu , huu ni mchezo mzuri ambao tumeuonyesha tangu niwe kocha wa Schalke, na iwapo wiki baada ya wiki tutafanya hivi , kuna uwezekano, wa kuwa na msimu mzuri wa Bundesliga".

Huko nchini Uingereza, mazungumzo wiki hii ni kuhusu kipigo ambacho ni cha kihistoria walichopata Arsenal London dhidi ya mabingwa watetezi wa Premier League Manchester United. Kipigo cha mabao 8-2 ikiwa ni mara ya pili Arsenal kupata kipigo kama hicho tangu mwaka 1896.

Lakini kocha wa Arsenal , Arsene Wenger ameahidi kumaliza mwanzo mbaya wa msimu huu wa fadhaa kwa timu hiyo kwa kutumia fedha ambazo zipo kununua wachezaji wengine baada ya kipigo hicho.

Wenger alishuhudia timu yake ya kuumba umba ikichanwa chanwa wakati Man United ikiwasambaratisha kwa ushindi mkubwa kabisa katika historia uwanjani Old Trafford jana Jumapili.

Arsene Wenger
Meneja wa Arsena Arsene Wenger akiangalia mchezo unavyoendelea.Picha: picture-alliance/ dpa

Hata hivyo Sir Alex Ferguson alimtetea hasimu wake mkubwa Wenger ,kwamba atafanikiwa kutoka katika maafa hayo, na wakati mgumu kabisa katika kipindi cha miaka 15 cha uongozi wake wa Arsenal.

Hata Pep Guadiola kocha wa Barselona ambao wamemchukua kiungo mahiri wa Arsenal Cesc Fabregas, amemtetea Arsene Wenger. Guadiola amesema kuwa ni vigumu kuamini kuwa kocha mwingine anaweza kufanya kama alivyofanya Wenger kwa Arsenal. Guadiola mwenye umri wa miaka 40 amesema kikosi kilichokwenda Old Trafford kilikuwa dhaifu mno kutokana na majeruhi na kumpoteza Fabregas pamoja na mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa Samir Nasri ambaye amejiunga na Manchester City.

Kwa upande mwingine ilikuwa ni siku mbaya kwa timu za mjini London wakati Manchester City nayo ilipoibomoa Tottenham Hotspurs kwa mabao 5-1. Liverpool ilikuwa na wikiendi nzuri baada ya kuichapa Bolton Wanderers kwa mabao 3-0, Chalsea ikaishinda Norwich City kwa mabao 3-1.

Nchini Hispania Cristiano Ronaldo alianzia pale alipoachia msimu uliopita kwa kupachika mabao 3 katika ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Real Zaragoza, wakati ligi ya Uhispania, La Liga ilipoanza rasmi baada ya mgomo wa wiki moja kufuatia mgomo wa wachezaji. Mabingwa wa Ulaya Barca wanaanza utetezi wao leo Jumatatu dhidi ya Villareal. Valencia iliishinda Racing Santander kwa mabao 4-3.

Huko Italia bado msimu haujaanza kutokana na mgomo wa wachezaji kutokana na mvutano kuhusiana na makubaliano mapya ya uhakikisho wa haki zao.Mgomo ulitangazwa siku ya Ijumaa baada ya mazungumzo baina ya chama cha wachezaji na Lega Serie A kuvunjika.

Wakati huo huo baada ya mwaka mmoja wa kashfa ambazo zimelitikisa shirikisho la soka la dunia FIFA, rais wa FIFA Sepp Blatter amesema jana kuwa atawasilisha mageuzi ya kupambana na rushwa mwezi Oktoba. Blatter ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa atatangaza agenda ya mageuzi yake baada ya mkutano wa tarehe 20-21 mjini Zurich na wenzake katika kamati kuu, ambapo wajumbe kadha ni washukiwa.

Fußball FIFA Präsident Sepp Blatter
Rais wa FIFA Sepp Blatter anataraji kutoa agenda ya mageuzi ya rushwa mwezi Oktoba katika mkutano wa kamati kuu.Picha: AP

Riadha, ubingwa wa dunia.

Ujerumani imefanikiwa kupata medali ya kwanza ya fedha katika michezo ya riadha ya ubingwa wa dunia kwa kurusha kitufe baada ya Nadine Müller jana Jumapili kirusha kitufe umbali wa mita 65.97. Ilikuwa ni furaha sana kwangu amesema Nadine Müller baada ya ushindi huo wa pili.

"Ilikuwa ni hali ya hisia kali, nilipiga kelele za furaha, kwamba kila kitu kimekwisha na ninarudi nyumbani na medali ya fedha . Ninafuraha kubwa , ni kitu cha kushangaza kwa kweli".

Wakati huo huo Usain Bolt anatarajia kuweka kando mwanzo mbaya katika mashindano ya ubingwa wa dunia baada ya kuondolewa katika mbio za mita 100. Hivi sasa anangalia ubingwa wa mita 200 fainali zitakazofanyika siku ya Ijumaa.

Leo kunafanyika fainali za mita 110 wanaume kuruka viunzi na mita 100 wanawake pamoja na mita 400.

Pia itakuwa mbio za nani zaidi kati ya Marekani na Jamaica katika mbio za mita 100 wanawake , ambapo Carmelita Jeter wa Marekani atakapopambana na Veronica Campbell-Brown wa Jamaica.

Jamaica hata hivyo hawatarajiwi kuwika sana katika mbio za mita 110 kuruka viunzi. Mshindi wa mbio hizo huenda akawa Liu Xiang wa China, Dayron Robles wa Cuba ama David Oliver wa Marekani .

Mbio za mita 400 wanawake zitakuwa pambano la Wamarekani wakati Allyson Felix akitafuta uwezekano wa kushindi medali nne za dhahabu wakati atakapopambana na Sandra Richards-Ross.

Tennis.

mashindano ya US open ya tennis yataanza leo Jumatatu kama yalivyopangwa baada ya kituo cha taifa cha Tennis kunusurika na uharibifu mkubwa wa kimbunga Irene, maafisa wamesema. Kimbunga hicho kimeukumba mji wa New York katika majira ya alfajiri jana Jumapili, na maeneo ya pwani yamefurika pamoja na maeneo ya mabondeni, lakini mji huo wenye watu wengi kabisa nchini Marekani umenusurika na uharibifu mkubwa ambao wengi walikuwa wakihofia.

Kwa taarifa hiyo ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari za michezo kwa leo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre/ape/afpe

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed