1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Litvinenko aliuliwa na majasusi wa Urusi?

21 Januari 2016

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa nchini Uingereza, huenda Rais Vladimir Putin aliidhinisha kuuliwa kwa aliyekuwa jasusi wa shirika la upelelezi la Urusi , KGB, Alexander Litvinenko, aliyetiliwa sumu jijini London.

https://p.dw.com/p/1Hhux
Aliekuwa jasusi wa Urusi ,Alexander Litvinenko
Aliekuwa jasusi wa Urusi ,Alexander Litvinenko,Picha: Reuters/V. Djachkov

Litvinenko aliekuwa na umri wa miaka 43 alikufa baada ya kunywa chai iliyotiwa madini hadimu, ya polonium kwenye hoteli ya mjini London ya Millenium.

Uchunguzi uliofanywa chini ya uongozi wa jaji wa mahakama kuu, Robert Owen umebainisha kwamba aliekuwa mpambe wa shirika la ujasusi la KGB, Andrei Lugovoy pamoja na mrusi mwengine, Dmitry Kovtun ndio waliomtilia sumu Litvinenko.

Inatuhumiwa kwamba majasusi hao walikuwa wanatekeleza agizo la shirika la ujasusi la Urusi lililochukua mahala pa shirika la zamani la KGB.

Akihutubia bungeni leo juu ya mkasa wa Litvinenko, waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Theresa May alisema kifo cha Litvinenko kilikuwa cha kushtusha sana.Amesema licha ya kuendelea kwa uchunguzi wa polisi hakuna mtu hata mmoja aliehusika na kifo chake aliechukuliwa hatua za kisheria.

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza bibi May amesema pana uwezekano mkubwa kwamba waliomwuua Litvinenko walikuwa wanalitekeleza agizo la shirika la ujasusi la Urusi FSB. Waziri huyo aliongeza kusema kwamba huenda Rais Vladimir Putin aliidhinisha mauaji hayo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Theresa May
Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Theresa MayPicha: picture-alliance/empics/J. Brady

Jaji wa Uingereza Robert Owen alieongoza uchunguzi pia amesema huenda Rais Putin aliidhinisha mauaji ya Litvinenko. Jaji Owen amesema anao uhakika kwamba majasusi wa Urusi, Lugovoy na Kovtun ndiyo waliomtilia Litvinenko sumu aina ya polinium namba 210.

Lakini Urusi imekanusha na imesema ripoti ya uchunguzi juu ya kifo cha Litvinenko itauathiri uhusiano baina ya nchi hiyo na Uingereza. Msemaji wa wizara ya mambo nje wa Urusi ameeleza kuwa uchunguzi uliofanywa na Uingereza haukuwamo katika msingi wa uwazi.

Msemaji huyo ameeleza kuwa mkasa wa Litvinenko unatumiwa kwa malengo ya kisiasa na serikali ya Uingereza.

Uchunguzi juu ya kifo cha Litvinenko ulianza mnamo mwezi Januari mwaka uliopitana mateoko yake yamechapishwa leo. Waziri wa mambo ndani wa Uingereza Bibi May amesema matokeo ya uchunguzi siyo jambo la kushangaza.Amesema matokeo hayo yanathibitsha tathmini za serikali za hapo awali kwamba mauaji ya Litvinenko yaliandaliwa na serikali ya Urusi.

Waziri huyo amesema serikali ya sasa nchini Uingereza pia inakubaliana na tathmini hiyo. Alexander Litvinenko aliekuwa mpinzani wa serikali, alikimbia Urusi mnamo mwaka 2000 na kuomba hifadhi ya kisiasa nchini Uingereza.

Mwandishi: Mtullya Abdu.rtrd,afp

Mhariri: Mohammed Khelef