1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Livepool dhidi ya Chelsea katika nusu fainali Champions League

Kalyango Siraj30 Aprili 2008

Je! Historia ya 2005 na 2007 itarudiwa?

https://p.dw.com/p/DrOu
Kocha wa Liverpool Rafael Benitez,anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuvunja daftari ya miaka mingi ya kutoifunga Chelsea nyumbani kwake Stamford Bridge.Liverpool na Chelsea wanakutana jumatano 30.04.08 London katika duru ya pili ya Champions League.Picha: AP

Nusu fainali ya pili katika kuwania kufuzu kwa fainali ya kombe la soka la Champions League bara la Ulaya,inafanyika leo mjini London kati ya watani wa jadi Chelsea dhidi ya Livepool .

Je! Yatakuwa marudio ya mwaka wa 2005 pamoja na mwaka jana,wakati Livepool mara zote hizo mbili ilikuwa ikiipiku Chelsea na kusonga mbele hadi fainali ya kombe hilo? Jibu litapatikana baada ya kipenga cha mwisho kulia leo jijini London na kuona ubao unasema nini.

Nazungumzia mkondo wa pili wa nusu fainali ya kombe la mwaka huu la Champinos League ambapo bila shaka fainali kwa vyovyote vile itakuwa fainali ya klabu za Uingereza tu kufuatia Manchester United kufuzu kwa fainali itakayofanyika mwezi Mei.

Man U, kama wanavyojulikana kimzaha na mashabiki wao wengi Afrika Mashariki na Kati, waliweza jana kuwalaza wenzao wa Uhispania Barcelona bao moja kwa nunge,bao lililopachikwa wavuni na Paul Scoles.

Sasa kijasho chembamba kinawasubiri wachezaji wa Liverpool na Chelsea. Si mara ya kwanza timu hizi zikikutana katika kombe hili na mkondo huu huu.Wakati Chelsea ilitupwa nje mapema sana mwaka wa 2006 na Barcelona,lakini Livepool iliwahi kuwanyima raha ya kucheza fainali mara mbili tena katika mkondo huu wa nusu fainali.Mwanzo ulikuwa mwaka wa 2005 na mara ya pili mwaka wa 2006.

Je mara hii historia itarudiwa.Anajibu swali hilo mwanasoka mashuhiri wa Tanzani Athuman China ambae sasa anaishi Uingereza

'Chelsea ni timu nzuri na inachezea kwao kwa hivyo inaweza ikashinda',aseme China.

Ili kubadili nadharia hiyo pamoja na kuwanyima wachezaji wa Chelsea uhondo wa fainali inabidi vijana wa Rafael Benitez, ambao mwenzangu mmoja hapa anawaita Bwawa la maini ,akimaanisha Livepool,itawabidi wafunge aidha bao au mabao kitu ambacho wamefanya mara moja tu katika mara zote tisa walizozuru Stamford Bridge chini ya uongozi wa kocha wao wa sasa.

Licha ya historia ya mara mbili lakini tayari wachezaji wa Livepool wameanza kupata tumbo joto.Mfano nahodha Steven Gerrard amekiri kuwa Chelsea ni timu nzuri licha ya kwenda sare ya kufungana bao moja kila upande walipokutana katika mkondo wa kwanza katika uwanja wa livepool wa Anfield.

Lakini bao la Chelsea lilikuwa la kujifunga wenyewe baada ya mlinzi wa Livepool,John Arne Riise, kuugonga mpira ndani ya lango lake badala ya kuoondoa.

Chelsea ikiwa inachezea nyumbani,itacheza kufa na kupona kuona kuwa angalau inafika fainali jambo ambalo haijalifanya katika historia ya klabu hiyo.

Hata hivyo Liverpool ambayo ilichukua kombe hilo mwaka wa 2005 na mwaka jana kufika fainali inatarajiwa kucheza kufa na kupona kuona kama inarejea fainali za Mei 21 mjini Moscow nchini Urusi.

Licha ya uhusiano kuwa mbaya kati ya uingereza na Urusi lakini Meya wa Moscow amesema leo jumatano kuwa mashabiki wa soka wa Uingeraza wataweza kuingia huko bila visa.

Hata hivyo mashabiki hao kila mmoja itambidi awe na tiketi yakuingia uwanjani pamoja na pasi halali ya kusafiria.

Licha kuwa fainali itakuwa ya klabu za uingerza lakini haijulikani kati ya Livepool na chelsea nai atafuzu,je Historia ya mwaka wa 2005 pamoja na ya mwaka wa 2007.hayo yatajulikana baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa na Refa Roberto Rosetti kutoka Italy akiwa katika uwanja wa Stamford bridge leo jioni jumatano.