1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Blair aionya Iran

30 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCEG

Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair amesema kuna hatua mbali mbali za kuifanya Iran kuwaachilia huru wanamaji wake 15 inaowashikilia.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Havier Solana ameongezea uzito kauli hiyo ya Blair kwa kusema kwamba Umoja wa Ulaya unaona hatua hiyo ya serikali ya Iran kuwa sio halali. Barua ya pili inayodhaniwa kuwa inatoka kwa mwanamaji pekee wa kike kati ya wanamaji wanaoshikiliwa inayoripotiwa kupelekewa mbunge wa jimbo lake inasema Uingereza inapaswa kujitowa nchini Iraq.Kama ilivyokuwa kwenye baruwa yake ya mwanzo mwanamaji huyo wa kike anasema kwamba yeye na wanamaji wenzake wanaoshikiliwa kwa bahati mbaya walipotea njia na kuingia kwenye eneo la bahari ya Iran.

Na habari za hivi punde zinasema Uingereza inatafakari kwa makini taarifa rasmi kutoka serikali ya Iran juu ya wanamaji wake 15 waliotekwa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uingereza amekataa kutowa maelezo zaidi juu ya taarifa hiyo ambapo amesema mara nyingi taarifa za aina hiyo huwa za siri lakini wataijibu rasmi serikali ya Iran hivi karibuni.

Taarifa hiyo ilipokelewa na ubalozi wa Uingereza mjini Tehran.