1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON Dalili za sumu ya Polonium 210 zagunduliwa katika sehemu kadhaa

28 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCom

Wachunguzi wa kifo cha kachero wa zamani wa Urusi aliyeuwawa kwa kupewa sumu Alexander Litvineko wamesema kwamba chembe chembe za sumu iliyotumika kumuuwa kachero huyo wa zamani zimegunduliwa katika sehemu kadhaa mjini London.

Watu watatu tayari wanashukiwa kuwa na chembe chembe hizo za sumu ya Polonium 210.

Ikulu ya Kremlin imekanusha kuwa rais Vladmir Puttin wa Urusi anahusika na kifo cha kachero huyo wa zamani.

Dalili ya chembe chembe za sumu hiyo zimepatikana nyumbani kwa Litvinenko, katika mkahawa alioutembelea na matokeo ya uchunguzi wa hivi punde yameonyesha kupatikana dalili hizo katika jumba lenye maofisi mjini London na katika eneo moja la matajiri katika wilaya ya Mayfair.

Alexander Litvinenko alikuwa akichunguza kifo cha mwandishi habari wa Urusi Anna Politikovskaya na shughuli za kampuni kubwa ya mafuta nchini Urusi. Yukos.