1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Mabaharia wa Uingereza wapongezwa

7 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCBe

Mabaharia 15 wa Uingereza walioachiliwa huru na Iran Jumatano iliyopita, wamepongezwa hii leo kwa tabia yao wakati walipokuwa wakizuiliwa mjini Tehran kwa siku 13.

Gazeti la Guardian la mjini London limeripoti leo kwamba kiongozi wa kanisa Katoliki baba mtakatifu Benedict XVI alimuandikia barua kiongozi wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, kumhimiza afanye kila juhudi ambazo zingeweza kusaidia wanamaji hao wa Uingereza kurejea nyumbani kwa sikukuu ya Pasaka.

Katika barua hiyo baba mtakatifu Benedict XVI alisema msaada wa Khamenei ungechukuliwa kuwa ishara muhimu ya kidini na ya ukarimu kutoka kwa umma wa Iran. Makao makuu ya kanisa katoliki mjini Vatican yamethibitisha kuwa baba mtakatifu aliiandika barua hiyo saa chache kabla mabaharia wote 15 kuachiliwa.

Balozi wa Iran nchini Uingereza, Rasoul Movahedian, ameitaka Uingereza ionyeshe ukarimu baada ya Iran kuwaachilia huru mabaharia hao.