1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Mtuhumiwa wa tano mbaroni

1 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBmk

Polisi imezipekua nyumba kadhaa karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Glasgow leo hii kuhusiana na shambulio kwenye uwanja huo na jaribio lililozimwa la kuripuwa mabomu yaliotegewa kwenye magari mjini London na imemtia mbaroni mtuhumiwa wa tano wa njama hizo za kigaidi.

Watu wanne wako mbaroni na watano yuko chini ya ulinzi hospitalini baada ya gari aina ya jeep kubamizwa na lango la kuingilia kwenye uwanja huo na kuripuka moto hapo jana.Polisi imekuwa ikifanya upekuzi kwenye nyumba kadhaa katika mji mdogo wa Houston nje ya Glasgow ambapo kwa mujibu wa majirani wanaume wawili wa asili ya Asia wamehamia hapo kama mwezi mmoja uliopita.

Polisi imesema imemkamata mtu watano leo hii huko Liverpool wakati watu wengine wawili mwanaume na mwanamke walikamatwa hapo jana wakiwa kwenye barabara kuu ya Cheshire kaskazini mwa Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown ambaye amesema Waingereza wanakabiliwa na tishio la muda mrefu na kuwataka wawe macho alikuwa na ujumbe huu ambao umeelekezwa kwa magaidi.

Anasema anafikiri ujumbe unaopasa kutoka Uingereza na kwa wananchi wa Uingereza ni mmoja: kwamba hawatosalimu amri, hawatotishwa na hawatomruhusu yoyote yule kudhoofisha mwenendo wa maisha wa Uingereza.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba mashambulizi hayo ya hivi karibuni kabisa yamekusudia kuishinikiza Uingereza kuondowa wananjeshi wake kutoka Iraq na Afghanistan.