1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Njama 30 za ugaidi zapangwa Uingereza

11 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCtx

Mkuu wa shirika la ujasusi la ndani nchini Uingereza amesema takriban kuna njama kuu 30 za kigaidi zinazopangwa kutekelezwa nchini humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa M15 Dame Manningham –Bulller amesema majasusi wake wanawafuatilia watuhumiwa 1,600 wengi wao wakiwa ni wazalia wa Uingereza wenye mafungamano na kundi la Al Qaeda nchini Pakistan.Amesema watu hao wanaojiandaa kujitolea muhanga maisha kwa kujiripuwa kwa kiasi fulani wanachochewa na hasira kutokana na kile wanachokiona kama sera dhidi ya Uislamu mathlan kujihusisha kwa Uingereza katika mizozo ya Iraq na Afghanistan.

Mkuu huyo wa ujasusi amefadhaishwa na idadi ya watu inayozidi kuongezeka kuwa tayari kufanya ugaidi kwa vitendo badala ya kuupendelea tu ambapo hutumbikizwa kwenye misimamo mikali au itikadi kali na marafiki,familia,katika mafunzo yalioandaliwa nchini Uingereza au nchi za nje,kutokana na picha za televisheni,mazungumzo ya vyumbani na kwenye tovuti za mtandao.

Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair amewaambia waandishi wa habari kwamba anakubaliana na tathmini hiyo ya shirika la ujasusi la M15.

Shirika hilo la ujasusi linasema limezima njama kuu tano za ugaidi tokea kuripuliwa kwa mabomu mfumo wa usafiri wa London hapo mwezi wa Julai ambapo watu 52 waliuwawa.