1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Uingereza kufichua ukiukaji wa haki za binadamu nchini Zimbabwe

20 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCH7

Zimbabwe imetishia kuwafukuza mabalozi wa mataifa ya magharibi. Uingereza imetangaza leo kuwa itaendelea kufichua ukiukaji wa haki za binadamu nchini Zimbabwe licha ya vitisho hivyo vilivyotolewa na serikali ya rais Robert Mugabe.

Serikali ya Mugabe inawalaumu wanadiplomasia hao kwa kuwaunga mkono wapinzani wanaotaka kuiondoa madarakani.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Zimbabwe, Simbarashe Mumbengegwi, amesema amewaonya mabalozi walio mjini Harare kwamba serikali haitasita kuwatimua watakaounga mkono siasa za upinzani.

Uingereza ambayo imethibitisha kuwa balozi wake mjini Harare ameonywa anyamaze kimya au afukuzwe, inajaribu kuushinikiza Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zichukue hatua kali dhidi ya utawala wa Zimbabwe.

Jana balozi wa Marekani nchini Zimbabwe, Christopher Dell, alitoka nje ya mkutano aliokuwa nao na waziri wa mashauri ya kigeni wa Zimbabwe.