1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LOS ANGELES:Upepo wapungua kasi California

25 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Cp

Mkasa wa moto katika jimbo la California nchini Marekani umeingia siku yake ya tano huku nyumba 1300 zikiteketea na watu yapata nusu milioni kulazimika kuyahama makazi yao.Wazima moto wanatumia kipindi hichi ambako pepo zimetulia kupambana na miale hiyo.

Eneo la kusini bado linaripotiwa kuwa na moto lakini kulingana na maafisa wa serikali viwango vya joto vilivyopungua pamoja na pepo zilizopungua kasi vyote vinachangia kusaidia kupambana na moto huo.

Rais George Bush wa Marekani aliyetangaza mkasa huo kuwa janga anatarajiwa kuzuru eneo hilo hii leo akiandamana na gavana wa jimbo la California Arnold Schwarzenegger.

''Natamani tungeweza kudhibiti upepo kwani jambo moja linaloathiri juhudi zetu za kuzima moto ni pepo kali za mgharaibi.Nimeelezwa kuwa huenda pepo hizo zikatulia na hilo basi litasaidia kupambana na moto kutumia vifaa tulivyonavyo.''

Shirika la kitaifa la kupambana na mikasa FEMA limepeleka maafisa wake alfu moja hususan kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi katika wilaya ya San Diego.Kwa upande mwingine wataalam wa kuzima moto wanaeleza kuwa kupungua kasi kwa pepo za Santa Ana kumeleta faraja ila pepo za bahari huenda zikasababisha hatari.Moto huo ulianza mwishoni mwa juma lililopita na mpaka sasa kuteketeza eneo lililo na ukubwa wa takriban kilomita alfu mbili na sabini na mbili.Watu sita wanaripotiwa kupoteza maisha yao na wengine zaidi ya sabini kujeruhiwa wengi wao wazima moto.