1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lufthansa na BA zasimamisha safari zao kwenda Misri

Zainab Aziz Mhariri: Lilian Mtono
21 Julai 2019

Mashirika ya ndege ya Uingereza British Airways na Lufthansa la Ujerumani yamesitisha kwa muda safari zao kwenda Cairo, Misri kutokana na wasiwasi wa kiusalama.

https://p.dw.com/p/3MREd
Deutschland British Airways und Lufthansa
Picha: picture-alliance/dpa/M. Mainka

British Airways ndio iliyoanza kwa kusimamisha safari zake kwa siku saba, kuanzia jana Jumamosi, kutokana na tahadhari iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Uingereza kwamba upo uwezekano mkubwa wa kufanyika mashambulio ya kigaidi. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imetoa tahadhari kwa raia wake wanaofanya safari kwenda Misri.

Shirika hilo la ndege la Uingereza limesema limesitisha safari zake kwa muda ili kutoa nafasi ya kufanyika tathmini kutokana na wasiwasi uliopo.

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imesema ndege zinazotoka Misri kwenda Uingereza zitawekewa hatua za nyongeza za kiusalama, huku ikiwataka abiria kutoa ushirikiano kwa maafisa wa usalama kwenye viwanja vya ndege. 

Wakati huo huo, shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa limesema lilisitisha safari zake za Misri kutokea Munich na Frankfurt siku ya Jumamosi ili kufuatilia hali hiyo ingawa limesema huenda likaanza tena safari zake Jumapili.

Pwani ya Sharm el Sheikh Cairo, Misri
Pwani ya Sharm el Sheikh Cairo, MisriPicha: picture-alliance/dpa/K. Elfiqi

Maafisa wa Misri ambao hawakutaka majina yao yatajwe, wamesema mashirika mengine ya ndege  yanaendelea na safari zao kama kawaida.

Utalii ndio chanzo kikuu cha mapato yanayoingiza fedha za kigeni nchini Misri. Sekta hiyo ilikuwa imeanza kunawiri tena baada ya maandamano makubwa yam waka 2011 kupinga utawala wa aliyekuwa Rais wan chi hiyo Hosni Mubarak aliyeondolewa madarakani pamoja na mashambulio ya mabomu ya mwaka 2015 yaliyoilenga ndege ya Urusi. Wengi kati ya abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo walikuwa wanatoka likizoni katika mji wa Pwani wa Sharm el-Sheikh.

Matukio mengine ni pamoja na kushambuliwa kwa kisu raia wa Ujerumani katika mji wa mapumziko maarufu wa Hurghada. Wajerumani wawili waliuawa na watalii wengine wanne walijeruhiwa.

Chanzo:/Permalink https://p.dw.com/p/3MQlo