1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahudumu wa ndege wa Lufthansa waanza mgomo

6 Novemba 2015

Shirika la ndege la Ujerumani la Lufthansa leo limefuta safari zake 290 baada ya wahudumu wa ndani ya ndege wa shirika hilo kutangaza mgomo wao kutokana na shirika hilo kushindwa kutimiza madai yao.

https://p.dw.com/p/1H1HM
Wafanyakazi wa Lufthansa
Wafanyakazi wa LufthansaPicha: picture-alliance/dpa/F. Rumpenhorst

Mgomo huo unafanyika baada ya uongozi wa Lufthansa kushindwa kufikia makubaliano na wafanyakazi wake katika suala la kuongezewa mshahara na kupinga mabadiliko katika mfumo wa kustaafu kwa wafanyakazi wanaostaafu mapema.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo imeeleza kuwa kiasi abiria 37,500 wataathirika na mgomo huo wa wiki nzima ulioanza majira ya saa saba mchana. Chama cha wahudumu wa ndani ya ndege-UFO, kimeitisha mgomo wa saa tisa, utakaoathiri safari za ndege zinazoingia na kutoka katika viwanja vya ndege vya Frankfurt na Duesseldorf, ingawa huenda maeneo mengine yakafuatia hapo baadae.

Hadi jioni ya leo, shirika la Lufthansa lilikuwa limefuta safari 290 za ndege, zikiwemo 23 zinazokwenda katika mabara mbalimbali, ambazo zinatakiwa kutua au kuondokea katika uwanja wa ndege wa Frankfurt. Lufthansa imesema asilimia 10 ya safari zote zitalazimika kufutwa.

Kiongozi wa UFO, Nicoley Baublies, ambaye anawawakilisha wahudumu hao wanaogoma, amesema wamejaribu kupunguza madhara ya mgomo huo kwa abiria wanaosafiri wakati ambapo shule zinakaribia kufunguliwa katika majimbo ya kusini ya Bavaria na Baden-Württemberg.

UFO haina tena muda wa kufanya mazungumzo

Baublies ameonya kuwa abiria wote wa Lufthansa wajiandae kupokea taarifa za kufutwa kwa safari zao katika dakika za mwisho. Ameongeza kusema kuwa kwa sasa chama chake hakina tena muda wa kufanya mazungumzo ya wazi na watasimamisha tu mgomo wao, iwapo Lufthansa itakubaliana na madai yao kwa kiwango kikubwa.

Kiongozi wa UFO, Nicoley Baublies
Kiongozi wa UFO, Nicoley BaubliesPicha: picture-alliance/dpa/F. Rumpenhorst

Lufthansa imesema inasikitishwa na kitendo hicho cha UFO na imeomba radhi kwa abiria wake, ikisema mgomo umetangazwa katika kipindi cha muda mfupi, hali iliyosababisha shirika hilo kushindwa kutoa taarifa kwa abiria wake katika wakati muafaka na kuwatafutia njia mbadala za usafiri.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Lufthansa, Carsten Spoehr, amesema shirika lake limeandaa vyumba 2,500 vya hoteli mjini Frankfurt kwa ajili ya abiria watakaoathirika na mgomo huo. Pia imeandaa mamia ya vitanda vya kukunja vitakavyowekwa kwenye viwanja vya ndege kwa ajili ya abiria wanaobadilisha ndege, hasa wale watakaoshindwa kupata visa zao.

Hata hivyo mashirika tanzu na washirika wa Lufthansa ya Germanwings, Eurowings, Lufthansa CityLine, SWISS, Austrian Airlines, Air Dolomiti na Brussels Airlines, hayotoshiriki katika mgomo huo.

Hii sio mara ya kwanza kwa Lufthansa kukumbwa na mgomo wa wafanyakazi wake, kwani marubani wa shirika hilo wameshawahi kugoma mara kadhaa tangu kuzuka kwa mzozo kati yao na uongozi wa shirika hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Daniel Gakuba