1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lukashenko amejipatia asilimia 83.49 ya kura

12 Oktoba 2015

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko ameshinda awamu ya tano ya urais, kwa mujibu wa matokeo ya mapema yaliyotolewa hii leo.

https://p.dw.com/p/1GmX4
Weißrusslands Präsident Alexander Lukaschenko
Rais wa Belarus Alexander LukashenkoPicha: Maxim Malinovsky/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi nchini humo, Rais Alexander Lukashenko amejipatia asilimia 83.49 ya kura zote katika uchaguzi uliofanyika jana.

Christian Haerpfer, Mkurugenzi wa shirika la utafiti la Eurasia Barometer aliyetangaza matokeo ya uchaguzi huo, amesema Alexander Lukashenko ameshinda uchaguzi huwo kwa kura za asilimia 80.3. Nafasi ya pili ameshika Tatiana Korotkevich kwa kura za asilimia 5.60 . Nafasi ya tatu ni Sergei Gaidukevich kwa kura za asilimia 5.10 na nafasi ya nne na ya mwisho ameshika Nikolai Ulakovich kwa asilimia1.90 tu ya kura jumla.

Uchaguzi huwo ulikuwa na mahudhurio ya wapiga kura ya asilimia 86.75, ya watu wote milioni saba waliojiandikisha kupiga kura.

Utawala wa miaka 21

Lukashenko mwenye umri wa miaka 61, ameiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1994. Watu kadhaa waliandamana jana katika mji mkuu wa Minsk kupinga matokeo hayo.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, kulizuka machafuko baada ya Lukashenko kushinda ushindi wa asilimia 80 ya kura zote, na mamia ya wafuasi wa upinzani waliwekwa kizuizini.

Belarus Wahlen 2015
Waandamanaji nchini BelarusPicha: Reuters/V. Fedosenko

Baada ya tukio hilo, Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani walikubaliana kuiwekea Belarus vikwazo vya kusafiri pamoja na kuizuilia fedha.

Uchaguzi wa hivi karibuni ni fursa kwa Lukashenko kuimarisha mahusiano na mataifa ya Umoja wa Ulaya. Alisema jana kuwa amepokea ripoti za Umoja wa Ulaya za kuzingatia kuregeza vikwazo ilivyoiwekea Belarus.

"Wamefahamu kuwa vikwazo vinapelekea madhara zaidi. Hatimaye wamekubali kuwa Belarus ni nchi ya kawaida," amesema Alexander Lukashenko.

Umoja wa Ulaya kuondoa vikwazo Belarus

Duru zimeliambia shirika la habari la afp, kuwa leo mawaziri wa nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuzingatia suala la kuiondolea vikwazo Belarus, na maamuzi kamili yanatarajiwa kufikiwa kabla ya Oktoba 31, ambapo hatua hizi zitamalizika muda wake na zitahitajika ama kuandikwa upya ama kufutwa kabisa.

Halikadhalika wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema kuwa uchaguzi huu ni jaribio litakaloweza kurejesha ushirikiano na Belarus, na wanatarajia ukandamizaji uliofanyika mwaka 2010 hautarudiwa.

Mchambuzi mmoja amesema kwamba Wabelarus wanasema matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo pamoja na waasi wa nchi jirani ya Ukraine wanaoungwa mkono na Urusi ni miongoni mwa sababu za kumchagua tena rais huyo aliyeko madarakani kwa mara ya tano.

Marekani iliwahi kumtaja Lukashenko kuwa dikteta wa mwisho barani Ulaya, na sasa kwa mara nyengine amepata mamlaka ya kuendeleza utawala wake wa miaka 21 katika nchi hiyo ya Ulaya ya mashariki.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/dpae

Mhariri:Iddi Ssessanga