1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lukashenko kukabiliwa na vikwazo vya EU?

Lilian Mtono
21 Septemba 2020

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wanakutana Jumatatu hii(21.09.2020) kujadiliana kuhusu iwapo wanaweza kuwawekea vikwazo idadi kubwa ya maafisa wa ngazi za juu wa Belarus.

https://p.dw.com/p/3imvk
Screenshot | Russland Sotschi Treffen Putin Lukaschenko | Alexander Lukaschenko
Picha: picture-alliance/Russian Look/V. Listsyn

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wanakutana Jumatatu hii(21.09.2020) kujadiliana kuhusu iwapo wanaweza kuwawekea vikwazo idadi kubwa ya maafisa wa ngazi za juu wa Belarus ambao ni pamoja na rais Alexander Lukashenko baada ya mpinzani mkuu wa rais huyo kuuomba Umoja wa Ulaya kuwa "majasiri zaidi" katika kuchukua hatua dhidi yake.

Umoja wa Ulaya umeorodhesha majina 40 ya watu ambao huenda wakakabiliwa na vikwazo ambavyo ni pamoja na mali zao kushikiliwa na zuio la kusafiri ikiwa na hatua zinazotokana na ushiriki wao katika udanganyifu wa kura za uchaguzi wa Septemba 9, uliompatia Lukashenko fursa ya kuongoza kwa awamu ya sita, lakini pia hatua kali dhidi ya waandamanaji zilizochukuliwa kufuatia matokeo hayo yanayozozaniwa.

Swali linalowakabili ni kuhusu iwapo watamuhusisha Lukashenko kwenye orodha hiyo. Lukashenko ameendelea kuchukua hatua zinazolenga kuukandamiza upinzani na vyombo huru vya habari katika kipindi chake cha miaka 26 ya utawala, lakini pia amekataa kata kata kuzungumza na waandamanaji. Baadhi ya mataifa ya Umoja huo wa Ulaya yanataka kuongezwa kwa mbinyo dhidi ya Lukashenko kwa kuongeza orodha ya vikwazo iwapo atakataa kuingia kwenye mazungumzo na upinzani.

Litauen Vilnius Belarus Oppositionsführerin Swjatlana Zichanouskaja
Mpinzani mkubwa wa Lukashenko, Swjatlana Zichanouskaja aiomba EU kuongeza nguvu BelarusPicha: Reuters/Ints Kalnins

Akizungumza baada ya baadhi ya mawaziri kukutana na mpinzani mkuu wa Lukashenko Sviatlana Tsikhanouskaya, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas alisema "machafuko ambayo Lukashenko ameyasababisha dhidi ya waandamanaji wanaoandamana kwa amani hayakubaliki kabisa".

Maas ambaye taifa lake linashikilia urais wa mzunguko wa Umoja wa Ulaya alisema mawaziri wanatakiwa "kujiuliza wenyewe swali kwa nini bwana Lukashenko, ambaye ana wajibu mkubwa zaidi asikabiliwe na vikwazo vya Umoja wa Ulaya"

Umoja wa Ulaya wakana kuingilia mambo ya ndani ya Belarus.

Tsikhanouskaya, anayeishi uhamishoni Lithuania baada ya kukimbia Belarus kwa hofu ya usalama wake na watoto wake, aliwaambia waandishi wa habari kwamba aliwaomba mawaziri hao kumsaidia. "Tulijaribu wenyewe kupambana na hali iliyopo, kwa nguvu zetu wenyewe Wabelarus, lakini sasa ninaelewa kwamba tunahitaji nguvu kutoka nje" alisema.

Aliiomba Ulaya kutomsaidia kifedha Lukashenko na serikali yake kwa sababu "italeta tu machafuko kwa kuwaua Wabelarus."

Mwanasiasa huyo mwanamke, alisema "vikwazo ni muhimu sana katika maüambano waliyonayo" ili kusaidia kuishinikiza serikali na kwa kuwa anatambua kwamba Ulaya inasita kufanya hivyo lakini "kwenye mkutano huu, ninawaomba kuwa majasiri zaidi."

Mkuu wa sera za kigeni wa Ulaya, Josep Borrell alisema mawaziri hao pia wataangazia kuhusu msaada wanaoweza kuutoa kwa watu w Belarus, lakini pia ni mahusiano ya aina gani wanatakiwa kuwa nayo na Minsk kwa kuzingatia kwamba "hatutambui uhalali wa urais wa Lukashenko nchini Belarus."

Aidha, amekana madai kuhusiana na uingiliaji wa Umoja wa Ulaya nchini belarus akisema "hilo haliwezi kuchukuliwa kama uingiliaji wa masuala ya ndani kwa sababu semokrasia na haki za binaadamu ni muhimu sana katika utambulisho wa Umoja wa Ulaya."

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uhispania Arancha Gonzalez Laya alisema kwamba ujumbe ambao Tsikhanouskaya ametupatia uko wazi: Tafadhali Ulaya ungeni mkono demokrasia na haki za binadamu nchini Belarus.

Mashirika: APE