1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Luxembourg. Viongozi wa umoja wa Ulaya wakiri kuwa umoja huo unakabiliwa na mzozo mkubwa.

19 Juni 2005
https://p.dw.com/p/CF1y

Waziri mkuu wa Luxembourg Jean Claude Juncker, ambaye hivi sasa anashikilia wadhifa wa rais wa umoja wa Ulaya , amekiri kuwa umoja huo umo katika hali mbaya ya mzozo.

Amesema hayo baada ya mkutano wa viongozi wa umoja wa Ulaya uliofanyika mjini Brussels kushindwa kukubaliana katika suala la bajeti ya muda mrefu hadi mwaka 2013.

Mazungumzo yalikwama baada ya kutokea kutokukubaliana juu ya matumizi ya hapo baadaye, suala la marejesho ya fedha za Uingereza pamoja na ruzuku inayotolewa na mataifa ya Ulaya kwa wakulima.

Kansela wa Ujerumani Gerhard Schroeder ameilaumu Uingereza pamoja na Uholanzi kutotaka kuridhia baadhi ya masuala na kusababisha kile alichosema kuwa ni mmoja kati ya mizozo mkubwa kabisa katika bara la Ulaya, suala ambalo limekanushwa na waziri mkuu wa Uingereza Bwana Tony Blair.

Wanasiasa wa umoja wa Ulaya pamoja na wachambuzi wa mambo sasa wanakubaliana kuwa kushindwa mara mbili katika suala la bajeti ya Ulaya na katiba huenda kutasubiri hadi mwaka ujao kuweza kutatuliwa.