1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 kujiondoa Goma?

27 Novemba 2012

Jeshi la Uganda amesema kundi la waasi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekubali kuwa waasi wataondoka mashariki mwa nchi hiyo katika miji ya Goma na Sake ambayo wamekuwa wakiishikilia.

https://p.dw.com/p/16qTR
Mpiganaji wa M23 akisimamia mkutano wa hadhara Goma.
Mpiganaji wa M23 akisimamia mkutano wa hadhara Goma.Picha: dapd

Kwa mujibu wa mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Aronda Nyakayirima, kiongozi wa tawi la kijeshi la M23, Kanali Sultan Makenga, amekubali kuondoa vikosi vya kundi hilo katika miji ya Goma na Sake iliyoko mashariki mwa Kongo.

Jenerali Nyakayirima alisema uamuzi uliofikiwa na viongozi wakuu wa nchi za Maziwa Makuu ni kuwa vikosi vya M23 viondoke mji wa Goma na Sake na viache azma yao ya kusonga mbele maeneo ya kusini.

Mkuu huyo wa jeshi aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba hatua hiyo ya kuviondoa vikosi vya M23 imeamuliwa itekelezwe bila ya masharti yeyote na kwamba madai ya kundi hilo yalizingatiwa na mkutano wa Kamati ya Kimataifa ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika Jumamosi iliyopita. Hakuna tamko lolote lililotolewa na waasi.

M23 wataka malalamiko yao yajadiliwe zaidi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Okello Oryem, alisema waasi wanataka malalamiko yao ambayo ni mengi yanayohitaji siku mbili au zaidi ili yajadiliwe na viongozi wa nchi za maziwa makuu, huku kwa sasa viongozi hao wakisema hatua ya vikosi hivyo kuikalia Goma ni kinyume na sheria.

Mkuu wa tawi la kisiasa la M23, Jean Marie Runiga.
Mkuu wa tawi la kisiasa la M23, Jean Marie Runiga.Picha: Michele Sibiloni/AFP/GettyImages

Hata hivyo, msemaji wa M23 amesema viongozi wake bado hawajasema lolote lakini suala la kuondoa vikosi mjini Goma sio kikwazo.

"Hatuelewi nini Uganda walizungumza na viongozi wetu, lakini kile ninachoweza kusema ni kuwa kuondosha vikosi eneo la Goma sio tatizo kubwa. Tunaweza kuviondoa hata sasa, jioni hii au hata muda wowote, " alisema Amani Kabasha alipokuwa akizungumza na Reuters.

Msemaji wa Serikali ya Congo Lambert Mende alisema hana shaka kuwa serikali ya Uganda imefanya mazungumzo na kiongozi wa waasi Sultan Makenga.

Mende amesema wameambiwa kuwa ombi la kuondosha vikosi vya M23 limekubaliwa, lakini kwa sasa wanasubiri matokeo ya uamuzi huo.

Jeshi la Kongo lajiandaa

Wakati huo huo, mkuu mpya wa majeshi ya ardhini nchini Congo, Jenerali Francois Olenaga, amesisitiza kwamba wanajiandaa kwa hali yoyote itakayotokea.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya (kulia), Rais Joseph Kabisa wa DRC (katikati) na Rais Yoweri Museveni wa Uganda katika mkutano kuhusu Kongo mjini Kampala, tarehe 24 Nov. 2012.
Rais Mwai Kibaki wa Kenya (kulia), Rais Joseph Kabisa wa DRC (katikati) na Rais Yoweri Museveni wa Uganda katika mkutano kuhusu Kongo mjini Kampala, tarehe 24 Nov. 2012.Picha: Getty Images

"Sichezi mchezo wa adui au marafiki. Sisi ni serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wa Congo. Sisi ni jeshi la taifa. Hatuwezi kufuata njia isiyo halali ya M23 au wale wanaowasaidia kutuhujumu. Wakongo wote wanajua kwamba tumeshambuliwa na tutachukua hatua dhidi ya mashambulizi," alisema Jenerali Olenaga wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Naye Mkuu wa tawi la siasa wa kundi la M23 Jean-Marie Runiga alitarajiwa kufanya mazungumzo na waandishi wa habari mjini Goma leo.

Mwandishi: Khatib Mjaja/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman