1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maadhimisho ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya vita vikuu vya kwanza vya dunia.

Sekione Kitojo11 Novemba 2009

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa walisimama pamoja kwa mara ya kwanza wakionyesha heshima kwa watu waliopoteza maisha yao katika vita vikuu vya kwanza vya dunia leo mjini Paris.

https://p.dw.com/p/KU4F
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kulia akimsalimu rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.Picha: AP

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa walisimama pamoja kwa mara ya kwanza leo Jumatano wakionyesha heshima kwa watu waliopoteza maisha yao katika vita vikuu vya kwanza vya dunia katika siku yalipofanyika makubaliano ya kusitisha vita, wakiweka mashada ya maua katika makaburi ya wanajeshi waliokufa vitani.

Hatuadhimishi ushindi wa mtu mmoja dhidi ya mwingine lakini ni madhila ambayo yalikuwa sawa katika kila upande, rais Nicolas Sarkozy amesema mbele ya kikosi cha jeshi na kundi la watu waliohudhuria.

Sarkozy na kansela Angela Merkel , katika hatua ya pamoja ya kuonyesha uhusiano wa karibu katika ya Ujerumani na Ufaransa, waliwasha moto katika makaburi hayo ya wanajeshi waliopoteza maisha yao katika mnara wa Champs Elysee.

Bendera za Ufaransa na Ujerumani zilipepea na bendi ya jeshi ilipiga nyimbo za taifa za Ujerumani na Ufaransa wakati viongozi hao wakiweka mashada ya maua na kuahidi kuwa mataifa yao hayatapigana tena vita dhidi yao.

Hatuwezi kufuta historia lakini kuna nguvu ambayo inaweza kutusaidia kuweza kuvumilia, nguvu ya maridhiano, Merkel amesema katika hotuba.

Kutokana na juhudi za maridhiano tumepata urafiki. Hakuna zawadi nzuri kama hii. Kwa zawadi hii ya urafiki kuna uwajibikaji wa pamoja, ambao unazidi kuongezeka kwa ajili ya mustakbali wa nchi zetu. Urafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani lengo lake liko katika umoja wa Ulaya.

Maadhimisho hayo yamekuja siku mbili baada ya Sarkozy kufanya ziara mjini Berlin ambapo alihudhuria pamoja na viongozi wengine wa Ulaya maadhimisho ya mwaka wa 20 tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin. Viongozi wa Ujerumani wamehudhuria matukio ya kumbukumbu nchini Ufaransa hapo kabla, hususan wakati kansela Helmut Kohl alipomshika mkono rais Francois Mitterrand mjini Verdun , eneo ambalo lilifanyika mapigano makali kabisa katika vita hivyo vya mwaka 1914-18.

Lakini ziara ya Merkel leo ilikuwa mara ya kwanza kwa kiongozi wa Ujerumani kuhudhuria sherehe hizo za siku ya makubaliano ya kuacha mapigano mjini Paris iliadhimisha kushindwa kwa Ujerumani baada ya miaka minne ya vita vilivyosababisha mamilioni ya watu kuuwawa.

Rais Sarkozy alimkaribisha kansela Merkel kwa maneneo ya ukaribu na maridhiano katika kumbukumbu hiyo hii leo.

Kansela Merkel leo umekuwa mgeni wa kihistoria, ambapo heshima umeidhihirisha heshima kwa Ufaransa na Wafaransa. iishi Ufaransa, iishi Ujerumani na uendelee urafiki wetu. hakutakuwa tena na vita baina yetu.

Viongozi hao wawili walisimama kimya kwa muda katika Arc de Triomphe, mahali panapo fanyika maadhimisho hayo, wakiwa pamoja na kikosi cha jeshi kinachoundwa na wanajeshi wa Ufaransa na Ujerumani , pamoja na maafisa wa jeshi kutoka nchi hizo mbili.

Tukio hilo la kukaa kimya saa 5 asubuhi tarehe 11 mwezi wa 11, linaadhimisha wakati miaka 91 iliyopita silaha zilinyamazishwa katika bara la Ulaya baada ya Ujerumani kutia saini makubaliano ya kusitisha vita na mahasimu wake.

Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE/DPAE

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman.