1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maadhimisho ya sherehe za muungano wa Ujerumani

3 Oktoba 2012

Maadhimisho ya siku ya muungano wa Ujerumani yameanza kwa ibada kubwa katika kanisa la Saint Michael mjini Munich.Siku kuu hii inatumiwa pia na waislamu wa Ujerumani kufunguwa milango ya misikiti yao.

https://p.dw.com/p/16JEh
Rais Joachim Gauck (wa pili kushoto) na spika wa bunge wanaelekea katika kanisa la St.Michael mjini MunichPicha: picture-alliance/dpa

Ibada katika kanisa la Saint Michael mjini Munich imeongozwa na askofu mkuu wa Munich na mji wa Freising, Kardinali Reinhard Marx, na askofu mkuu wa kanisa la kiinjili la jimbo la Bavaria, Heinrich Bedford-Strohm, kwa ushirikiano pamoja na askofu wa kanisa la Kiorthodox, Augoustios.

Zaidi ya watu 1500, viongozi wakuu wote wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na rais Joachim Gauck , kansela Angela Merkel,na waziri mkuu wa jimbo la Bavaria, Horst Seehofer,wameshiriki katika ibada hiyo itakayofuatiwa baadae leo mchana na sherehe rasmi katika jumba la Opera la taifa ambako spika wa bunge, Nobert Lummert, anatazamiwa kutoa hotuba ya ufunguzi wa sherehe hizo.

Mwanzoni mwa ibada hiyo ya kuadhimisha siku ya muungano, askofu mkuu wa Munich na Freisig, Kardinali Reinhard Marx, alitoa mwito kuweko mshikamano barani Ulaya. Kardinal Marx amekumbusha "muungano wa Ujerumani usingewezekana bila ya ushirikiano wa Ulaya." Amekumbuka yaliyotokea miaka 22 iliyopita na kusisitiza kwa kusema "ilikuwa kama miujiza mipaka ilipofunguliwa". "Muungano ni dalili ya hali ya kuaminiana na kuwaamini majirani na ni kitambulisho cha utayarifu wa kufuata kwa pamoja njia mpya barani Ulaya. La muhimu zaidi ni kuwa na mtazamo wa aina mpya wa Ulaya utakaopundukia masuala ya sarafu, uchumi na fedha", ameshadidia Kardinali Marx ambae pia ni mwenyekiti wa baraza la maaskofu barani Ulaya.

Tag der Deutschen Einheit
Askofu mkuu wa Munich na Freising,kadinali Reinhard Marx (kushoto) pamoja na rais Joachim Gauck na waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer(kulia)Picha: dapd

Kwa ushirikiano pamoja na askofu mkuu wa kiinjili katika jimbo la Bavaria, Heinrich Bedford-Strohm, wakuu hao wa kidini wamewatolea mwito wajerumani wachangie kuifanya dunia iwe bora. Wamewatolea mwito pia wanasiasa wazingatie yanayotokea duniani wanapopitisha maamuzi yao.

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, ametoa mwito wa kuendelezwa juhudi za kuiunganisha Ulaya licha ya mgogoro wa sarafu ya Euro. Waziri Westerwelle amekosoa "hisia za kujipendelea kitaifa na itikadi kali na kusema hisia kama hizo ni hatari katika dunia inayobadilika.

17.09.2012 DW DEUTSCHLAND HEUTE Imam Ali Moschee
Msikiti wa Imam AliPicha: DW

Wakati huo huo, na kama kawaida yake mnamo siku ya leo ya sherehe za muungano wa Ujerumani, misikiti zaidi ya 600 ya humu nchini imeacha wazi milango yao kuwakaribisha waumini wa dini zote nyengine. Watu zaidi ya laki moja wanatarajiwa kuitembelea misikiti hiyo. Mpango wa misikiti kuacha milango wazi umeanza tangu mwaka 1997. Lengo ni kuhimiza hali ya kuelewana kati ya waumini wa dini tofauti.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/dpad/epd/KNA

Mhariri: Miraji Othman