1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafa ya Japani hayana kifani

13 Machi 2011

Wakati Japani taifa lenye nguvu kubwa kiuchumi duniani likiwa mbioni katika jitihada za uokozi, mamia kwa mamia ya miili watu waliouwawa imeendelea kupatikana.

https://p.dw.com/p/10YOg
Moshi umeonekana katika kiwanda cha Daiichi, Fukushima.Picha: AP

Idadi ya vifo kutokana na tetemeko kubwa la ardhi la kipimo cha richter cha 8.9 nchini Japani inaweza kupindukia 10,000 katika mkoa mmoja pekee wa Miyagi. Serikali ya nchi hiyo inaendelea na juhudi za uokozi pamoja na kuwaondolea wasi wasi wananchi wake juu ya uwezekano wa kuvuja kwa sumu ya miale ya nuklea katika mitambo yake miwili ya nuklea ilioharibiwa kutokana na tetemeko hilo.

Japan Erdebeben Tsunami
Picha: AP

Hadi sasa imethibitishwa watu 800 wamekufa huko Miyagi na katika maeneo mengine kaskazini mashariki mwa Japani ambayo Ijumaa imepigwa na tetemeko hilo la ardhi lililoandamana na mawimbi makubwa ya tsunami.Hadi sasa kumekuwa hakuna mawasiliano na watu hao 10,000 ambao hawajulikani walipo katika mji wa Minaminsariku huko Miyagi.

Awali polisi ilisema zaidi ya watu 2,000 wameuwawa au hawajulikani walipo katika mikoa ilioathirika.

Afisa wa serikali ya mitaa katika mji wa Futaba ulioko mkoa wa Fukushima ameliambia shirika la habari la Kyodo kwamba asilimia 90 ya nyumba katika maeneo matatu ya watu wanaoishi katika mwambao yamesombwa na mawimbi ya tsunami.

Japan Erdbeben
Picha: AP

Takriban watu 390,000 wamekimbia nyumba zao wengi wao wakijipatia nafasi ya kujistiri katika vituo vya kujihafadhi kwa dharura vya jamii na katika mashule.

Serikali inawatuliza wananchi

Wakati huo huo afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Japani amesema hakuna matatizo kuhusiana na mtambo wake wa nuklea ulioharibiwa hata kama kuna kiwango fulani cha sumu ya miale ya nuklea kiliovuja.Maafisa hivi sasa wanaendelea na juhudi za kuzuwiya kupanda kwa kiwango cha joto kupindukia katika mtambo wake huo.Serikali inasema mtambo wake mwengine wa nambari tatu pia uko katika hatari ya kuripuka kama ilivyotokea katika mripuko wa mtambo wake nambari moja.

Fukushima 2011 Bevölkerung
Picha: picture-alliance/dpa

Katibu wa Baraza la Mawaziri la Japani Yukio Edano amesema hakuna hatari kwa wakaazi wanaoishi karibu na mtambo huo na hata kama mripuko utatokea kontena lenye kuhifadhi nishati ya nuklea linaweza kuhimili mripuko huo.

Mitambo mwili nambari moja na nambari mbili huko Fukushima kama kilomita 240 kaskazini mwa Tokyo ilipoteza uwezo wao wa kutoa ubaridi baada ya tetememko hilo la ardhi kusababisha kukatika kwa umeme wa majenereta ya umeme na yale yenye kusaidia yaliokuwa yakipoza mitambo hiyo.

Hapo jana mripuko umeharibu jengo lenye mtambo nambari moja na kujeruhi watu wanne. Watu 22 wamelazwa hospitali baada kuonekana kuathirika na miale ya nuklea iliovuja kutoka mtambo huo juu ya kwamba haikuweza kujulikana mara moja watu hao wameathirika kwa kiasi gani na hivi sasa wako katika hali gani.

Takriban watu 200,000 wamehamishwa umbali wa kilomita 20 kutoka kanda ya salama karibu na mitambo hiyo.

Japani imetowa wanajeshi wake 200,000 kama asilimia 40 ya kikosi chake cha ulinzi kuongoza juhudi ngumu za uokozi na mamia ya meli,ndege na magari yamekuwa yakielekea katika mwambao wa Pasifiki.

Mwandishi:Mohamed Dahman
Mhariri:Hamidou Oumilkher