1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wahukumiwa kwa uzembe Afghanistan

Mjahida 19 Mei 2015

Maafisa 11 wa Afghanistan wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kushindwa kumlinda mwanamke aliyepgwa hadi kufa na kundi la watu mjini Kabul baada ya kuhusishwa kimakosa na kitendo cha kukufuru.

https://p.dw.com/p/1FRqe
Mahakama iliyotoa hukumu kwa maafisa hao wa polisi mjini Kabul
Mahakama iliyotoa hukumu kwa maafisa hao wa polisi mjini KabulPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Khan

Hukumu hiyo imetolewa baada ya wanaume wanne wa Aghanistan kuhukumiwa kifo, huku wengine wanane wakihukumiwa miaka 16 jela mapema mwezi huu kwa mauaji ya mwanamke huyo kwa jina Farkhunda aliyekuwa na miaka 27.

"Mmehukumiwa kutokana na uzembe wa majukumu yenu, mwaka mmoja jela," alisema jaji Safiullah Mojaddidi kwa washitakiwa hao 11 waliojumuisha maafisa wakuu wa polisi. Hata hivyo maafisa wengine wanane hawakupatikana na hatia. " Uamuzi huu sio wa mwisho washitakiwa wana haki ya kukata rufaa," aliongeza jaji Safiullah Mojaddidi.

Baadhi ya walioshitakiwa kwa mauaji ya Farkhunda
Baadhi ya walioshitakiwa kwa mauaji ya FarkhundaPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Gul

Kundi la watu waliojaa hasira walimshambulia Farkhunda tarehe 19 mwezi Machi, kwa kumpiga vibaya na kumchoma moto karibu na mto Kabul. Baada ya tukio hilo watu 49 walikamatwa wakiwemo maafisa 19 wa polisi.

Kutokana na mikanda ya video iliochukuliwa na watu waliokuwa karibu, polisi hao walionekana wakisimama tu katika eneo la tukio bila kuchukua hatua zozote za kulizuwiya kundi hilo kumpiga Farkhunda.

Shambulizi hilo lilitokea baada ya muuzaji mikufu alipomtuhumu Farkhunda kimakosa kuchoma kitabu cha Koran. Mauaji yake yalisababisha maandamano nchini Afghanistan na kuzua hisia mbali mbali duniani juu ya namna wanawake wa Afghanistan wanavyodhulumiwa.

Mchakato wa kuendesha kesi hizo wakosolewa

Licha ya kupongezwa hukumu hizo za kwanza za aina hiyo nchini Afganistan pia kulikuwa na wasiwasi juu ya usawa wake. Kwa upande wake shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch lilisema linawasiwasi juu ya namna kesi hizo zilivyoendeshwa kwa kuwa wengi wa washitakiwa walikosa mawakili wa kuwawakilisha.

Maandamano ya kutaka haki kwa msichana Farkhunda aliyeuwawa na mjini Kabul
Maandamano ya kutaka haki kwa msichana Farkhunda aliyeuwawa na mjini KabulPicha: DW/H. Sirat

Awali Heather Barr, mtafiti mkuu katika shirika moja la kutetea haki za wanawake barani Asia, amesema kesi hii inatoa hisia kwamba serikali ya Afghanistan inataka kufanyika mchakato wa haraka wa kuitoa kesi hii nje ya vyombo vya habari na kusonga mbele, badala ya kuishughulikia ipasavyo na kuchunguza kwa haki ni kwa namna gani tukio kama hili linaweza kutokea.

Kesi hii ya Farkhunda inaangazia hali ya ukatili inayoendelea kwa wanawake wa Aghanistan licha ya mabadiliko kufanywa tangu utawala wa Taliban ulipoanguka mwaka wa 2001.

Wakati huo huo ripoti ya Umoja wa Mataifa imeihimiza serikali ya nchi hiyo kuimarisha upatikanaji wa haki kwa waathiriwa wa kike wanaopitia ukatili.

Kwa sasa kesi nyingi za ukatili dhidi ya wanawake zinasuluhishwa kupitia upatanishi hii ikionyesha mapungufu yaliopo katika mfumo wa makosa ya jinai ikiwemo madai ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Mwandishi Amina Abubakar/ afp/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman