1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaelekea wapi

3 Novemba 2015

Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Uturuki bado yanawashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani sawa na wanavyoumulika mzozo wa wakimbizi na jinsi unavyowasumbuwa wanasiasa wa humu nchini

https://p.dw.com/p/1GykM
Wafuasi wa Erdogan wakisherehekea baada ya ushindi wa chama chao cha AKPPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Malla

Tuanze lakini na uchaguzi mkuu wa Uturuki na matokeo yake.Gazeti la "Schwäbische Zeitung" linamulika jinsi rais wa Uturuki anavyojivunia uungaji mkono miongoni mwa waturuki wanaoishi humu nchini.Gazeti linaendelea kuandika:

"Recep Tayyip Erdogan ana wafuasi wengi kabisa Ujerumani.Mtoto huyo wa fundi viatu kutoka Anatolia,anavutia umati wa watu tangu katika kumbi za mikutano mpaka viwanjani anapofanya kampeni zake za uchaguzi.Kwamba mpaka nyumbani chama cha Haki na Maendeleo AKP kimefanikiwa kujikingia wingi wa kustaajabisha wa kura,waturuki wanaoishi nchini Ujerumani wanaliangalia hilo kuwa ni faraja.Msimamo wa serikali kuu ya Ujerumani kuelekea kiongozi huyo wa mjini Ankara anaehitajika ili kusamimia wimbi la wakimbizi,nao pia unaangaliwa kwa jicho jema.Hata hivyo watu wanabidi wawe na tahadhari mbele ya bwana huyo na chama chake ambao hawathamini maadili ya magharibi linapohusika suala la uhuru wa vyombo vya habari,hali ya uwazi na kutenganisha shughuli za serikali na dini.Ingawa hii leo Erdogan amepata nguvu kupita kiasi kutokana na matokeo ya chama chake katika uchaguzi mkuu uliopita na pia kutokana na umuhimu anaopewa katika kulishughulikia suala la wakimbizi,hata hivyo hali hiyo isimfanye akasahau umuhimu wa kuleta suluhu katika jamii au kujaribu kujongelea maadili ya magharibi."

Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linamulika mustakbal wa Uturuki baada ya uchaguzi na kuandika:

"Wapi inaelekea Uturuki,suala hilo litategemea kama serikali mpya ya chama cha AKP itatekeleza kile ilichoahidi yaani kuwanyooshea mkono wakurd na pia kukomesha mashambulio dhidi ya PKK.Kama watafanikiwa kupunguza mwanya mpana ulioko kati ya wafuasi wake wanaofuata msimamo mkali wa kihafidhina na wale wanaoelemea upande wa magharibi.Na kama Erdogan atataka kwa kila hali kutekeleza ndoto yake ya kugeuka rais mwenye madaraka makubwa kabisa.Uturuki haijaacha bado kuzusha maajabu.

Mzozo wa waakimbizi wawatia kishindo wanasiasa

Mada ya mwisho magazetini inahusiana na mzozo wa wakimbizi na jinsi unavyoathiri serikali kuu ya muungano mjini Berlin.

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika:

"Katika sera ya wakimbizi bado hapajapatikana ufumbuzi wa haraka kuhusu matatizo yaliyoko.Vyama vikuu vinasaka njia ya namna ya kuwasaidia wale wanaotokea katika maeneo ya vita wanaoomba kinga ya ukimbizi,naiwe nchini Ujerumani au kwengineko-njia ambayo itapelekea wasitie kabisa mguu wao humu nchini.Kwasasa yadhihirika kana kwamba kuna mashindano ya nani atakuja na fikra bora au kali kuliko zote.Mwishoe wanasiasa ndio wanaoonekana wamezidiwa.Mikururo ya wakimbizi ni changamoto kwa Umoja wa ulaya,na sio tu kwa Ujerumani inayofanya kila la kufanya ili kulinda hadhi ya Ulaya.Huo ni mchango mkubwa mbali na kuwajibika kimataifa katika kuleta amani katika maeneo yanayaosumbuliwa na vita.Yote mawili ni tete na yenye kuhitaji subira.Hata hivyo msaada wa haraka unahitajika na sio mivutano ya kisiasa inayotanguliza mbele mikakati ya vyama badala ya ufumbuzi wa maana.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman