1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya HIV yaongezeka Ulaya mashariki na Asia ya Kati

Sylvia Mwehozi
24 Julai 2018

Dawa zinazotumiwa kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) hufanya kazi pale zinapotumiwa haraka kabla na baada ya kujamiiana vilevile na wakati zinapotumika kwa muda mrefu.

https://p.dw.com/p/321Vn
HIV-Selbsttest
Picha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Tafiti za kitabibu zilizowasilishwa siku ya Jumanne katika mkutano wa kimataifa wa masuala ya Ukimwi mjini Amsterdam zinaonesha hivyo. Matokeo kutoka nchi nyingi yanathibitisha tafiti zilizopita juu ya ufanisi wa vidonge vya kuzuia maambukizi ya Ukimwi (PrEp). Wanaume walioshiriki mapenzi na wanaume wenzake bila ya kutumia mipira ya kuzuia maambukizi kondomu, hawakupata maambukizi wakati walipomeza vidonge. Utafiti mwingine ulibaini kwamba mwanamme aliye na maambukizi ya VVU hakuambukiza virusi kama akitumia vidonge vya PrEp kila siku.

Chini ya PrEp, vidonge vya kupambana na VVU ambavyo awali vilitumika katika matibabu ya mgonjwa aliye na maambukizi hutumiwa kwa watu walio na afya ili kuzuia maambukizi. Vidonge hivyo vinasaidia kuzuia virusi kutojizalisha ndani ya seli.

PrEP - Medikamente zur Vorbeugung von HIV
Kidonge cha PrEP kinatumika kuzuia maambukizi ya HIV kabla na baada ya kujamiianaPicha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Watafiti pia wanapendekeza kwamba wakati bado hakujawa na mafanikio ya kutafuta chanjo ya VVU, utafiti wa muda mrefu unaonyesha matokeo yenye matumaini. "Hizi ni zama mpya katika kuzuia VVU", alisema Linda-Gail Bekker ambaye ni rais wa  Jamii ya Kimataifa ya VVU katika mkutano huo wa Amsterdam ulioanza siku ya Jumatatu.

Mwanasayansi mwandamizi kutoka Marekani Daktari Anthony Fauci ameyaita matokeo ya tafiti hizo kuwa yenye "kutia moyo" na "kushangaza".

Maambukizi mapya duniani

Kiasi ya watu milioni 36 duniani kote wana maambukizi ya VVU na mengine mapya milioni 1.8 hutokea kila mwaka, anasema Fauci ambaye pia ni mkurugenzi wa taasisi ya taifa ya mzio na magonjwa ya kuambukiza. "Njia pekee ya kupunguza kuenea ni kwa kuzuia visa vipya vya maambukizi", alisema.

Fauci anasema kupanua upatikanaji wake sio suala tu la kibinadamu bali pia ni sera nzuri. Hadi ipatikane chanjo, mipira ya kondomu ndio njia bora pekee ya kujikinga na VVU, lakini si kila mmoja anaitumia au anafanya hivo kila wakati, kwahiyo njia nyingine zinahitajika.

Maambukizi ya VVU Ulaya Mashariki na Asia

Niederlande Amsterdam - Prinz Harry zur 22. Internationalen AIDSKonferenz
Mwanamfalme wa Uingereza Prince Harry(kulia) katika mkutano wa masuala ya HIV mjini AmsterdamPicha: Reuters/Y. Herman

Karibu watu 190,000 wanaambukizwa VVU Ulaya Mashariki na Asia ya Kati kila mwaka, na karibu asilimia 80 wanaishi nchini Urusi kwa mujibu wa mashirika sita. Shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na Ukimwi la UNAIDS, lilitoa idadi ya maambukizi 130,000 kwa mwaka, lakini lilikubaliana kwamba Ulaya mashariki na Asia ya Kati kumeshuhudiwa ongezeko la maambukizi.

Hali ilivyo kusini mwa Sahara

Ukosefu wa kutambua maambukizi ya VVU ni hatari kubwa miongoni mwa vijana walioko nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, kulingana na wataalamu. Hadi robo tatu ya vijana walioambukizwa VVU katika nchi hizo hawafahamu hali zao.

Umoja wa Mataifa ambao unataka kutokomeza maambukizi ya Ukimwi ifikapo 2030, hivi karibuni ulionya kwamba idadi ya maambukizi mapya inazidi kuongezeka katika nchi nyingi hususan Ulaya mashariki na Asia. Mwaka jana watu milioni 1.8 waliambukizwa VVU, ambavyo vinasababisha upungufu wa kinga mwilini kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Kila mwaka watu karibu milioni 1 hupoteza maisha kwasababu ya maradhi yanayohusishwa na VVU.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/ap/afp

Mhariri: Mohammed Khelef