1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano dhidi ya Rais Barrow yafanyika Gambia

Amina Mjahid Daniel Gakuba
16 Desemba 2019

Adama Barrow ameshindwa kutimiza ahadi yake ya kuachia ngazi kama rais wa Gambia baada ya miaka 3 na sio miaka mitano. Katiba ya nchi hiyo inamkinga lakini raia wanamshinikiza kutimiza ahadi yake na kuondoka madarakani.

https://p.dw.com/p/3UucQ
Gambia Protest gegen Präsident Adama Barrow, Rücktrittsforderung
Picha: DW/O. Wally

Raia wa Gambia wanaandamana kufuatia hatua ya Rais Barrow kuendelea kubakia madarakani licha ya ahadi yake kuwa ataiongoza nchi hiyo kwa miaka mitatu tu na sio zaidi. Raia wa taifa hilo wamegadhabishwa na hatua yake ya kushindwa kutekeleza maelewano yake na muungano wa vyama nchini humo vilivyompa nafasi hiyo ya kuiongoza Gambia kwa miaka mitatu.

Hatua ya kuzungumza dhidi ya rais ni kitu kilichokuwa hatari nchini Gambia lakini leo wengi wameazimia kutumia haki yao ya kuandamana kutaka rais huyo kuwajibika.

Gambia iliingia katika mgogoro wa kikatiba mwenzi Desemba mwaka 2016 baada ya Rais Barrow kumshinda rais Yahya Jammeh katika uchaguzi wa rais, lakini kiongozi huyo wa muda mrefu Jammeh akagoma kung'atuka  madarakani hatua iliyoilazimisha Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS ikiungwa mkono na Umoja wa Mataifa kujitayarisha kuuingilia kijeshi mgogoro huo.

Barrow pamoja na muungano wa vyama vingine vya kisiasa  na makundi ya kiraia, wakawa na makubaliano ya kumaliza mgogoro huo na tarehe 19 mwezi Januari mwaka 2017 Barrow akiwa na ujuzi mdogo wa kisiasa akaapishwa kama rais wa mpito akiwa katika nchi jirani ya senegal, siku kadhaa baadaye Jammeh akakimbilia uhamishoni na Barrow akarejea nyumbani kuiongoza nchi.

Barrow aonekana kubadilisha mipango ndani ya muungano wa vyama

Gambia Präsident Adama Barrow kündigt Wahrheitskommission an
Rais wa Gambia Adama BarrowPicha: picture-alliance/AP Photo

Kulingana na Peter Penar mkurugenzi wa taasisi ya viongozi wa Afrika na profesa katika chuo kikuu  cha Davidson College  katika jimbo la North Carolina, nchini Marekani Barrow anaonekana kubadilisha mipango ndani ya muungano, Katiba ya Gambia inakubali rais aliyechaguliwa kumaliza muhula wake na hilo ndilo rais huyo analolipigania.

Huku muda wake wa miaka mitatu ukikaribia kumalizika, vuguvugu jipya linaloitwa "Miaka mitatu imemalizika" limeanzishwa kwa nia ya kuwawajibisha viongozi wa Gambia. Barua iliyoandikwa kwa mkono inayomtaka Barrow kuondoka madarakani ifikapo Januari 19 itawasilishwa kwa serikali mjini Banjul hii leo.

Raia wa Gambia hawafahamu kile kitakachotokea mbeleni lakini kile kinachoonekana wazi ni kwamba mashirika ya kiraia yamezidi kupata nguvu, na pia kuna wasiwasi wa iwapo Barrow ataachia madaraka basi huenda kukatokea kipindi cha hatari cha pengo la uongozi hadi pale uchaguzi mwengine utakapoitishwa.

Chanzo DW