1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano kuhusu wahamiaji yaigawa Ulaya

13 Septemba 2015

Mamia kwa maelfu ya wakaazi wa Ulaya waandamana Jumamosi(12.09.2015)kuunga mkono na wengine wakipinga mmiminiko wa wakimbizi, wakati Munich mji wa Ujerumani ukiemewa na wimbi hilo la jipya la wakimbizi.

https://p.dw.com/p/1GVkr
Maandamano ya kuunga mkono wakimbizi London (12.09.2015)
Maandamano ya kuunga mkono wakimbizi London (12.09.2015)Picha: Reuters/K. Coombs

Ikionekana kama nchi ya hali bora ya maisha na wengi wa wale wanaotaka hifadhi bora barani Ulaya , zaidi ya wakimbizi 9,000 wamemiminika nchini Ujerumani , katika mji mkuu wa jimbo la Bavaria Munich jana Jumamosi pekee.

Wengi zaidi wametarajiwa kuwasili , na kusababisha maafisa wa mji huo kuonya kuwa mji huo wa kusini unaelemewa kupita kiasi na utapata taabu kupata vitanda kwa wakimbizi wote wapya.

Tofauti zajitokeza kwa wakaazi wa Ulaya

Wakati bara hilo linahangaika kushughulikia wimbi kubwa kabisa la wahamiaji tangu vita vikuu vya pili vya dunia , tofauti kubwa zimejitokeza baina ya mataifa 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya , kwa upande wa serikali na mitaani pia.

Mjini London , mamia kwa maelfu waliandamana katika mji huo wakibeba mabango yanayosema "Maisha ya wakimbizi ni muhimu" na "Hakuna binadamu asiyeruhusiwa kisheria".

Jeremy Corbyn (katikati ) kiongozi mpya wa chama cha Labour nchini Uingereza.
Jeremy Corbyn (katikati ) kiongozi mpya wa chama cha Labour nchini Uingereza.Picha: Reuters/S. Wermuth

Kiongozi mpya wa chama cha Labour aliyechaguliwa hivi karibuni na mwanasiasa mkongwe wa mrengo wa shoto Jeremy Corbyn amevutia kundi kubwa la watu na kushangiriwa wakati alipokuwa akilihutubia kundi la watu akiwa nyuma ya lori.

"Fungueni mioyo yenu na fungueni akili zenu," mkuu huyo wa chama cha upinzani amesema, "kuelekea kuwasaidia watu ambao ni wahitaji, wanaohitaji mahali salama kuishi, wanataka kuchangia katika jamii yetu, na ni binadamu kama sisi wote."

Wajitokeza kuonesha mshikamano

Mjini Copenhagen , watu 30,000 walijitokeza kuelezea mshikamano wao na watu wanaoomba hifadhi, wakati maandamano kama hayo yamehudhuriwa na maelfu ya watu katika mitaa ya Madrid na Hamburg.

Wahamiaji wanaowasili katika mji wa Munich nchini Ujerumani.
Wahamiaji wanaowasili katika mji wa Munich nchini Ujerumani.Picha: Reuters/M. Rehle

"Nataka kuunga mkono wakimbizi," amesema Deborah Flatley katika maandamano mjini London, akibeba bango alilolitengeneza mwenyewe lenye maandishi: "Tunavutiwa na ushujaa wenu. Mnastahili maisha salama na ya furaha. Tunawakaribisha hapa kwa mikono miwili".

Kijana wa kiume aliyevalia kama dubu la Paddington ---aliyewasili katika kituo cha treni mjini London cha Paddington akitokea katika maeneo ya kijijini ya Peru , katika kitabu mashuhuri cha Michael Bond --akishika bango lililoandikwa : "Dubu wa Paddington alikuwa mkimbizi".

Mjini Berlin, waandamanaji walibeba bendera ya Syria Ikiwa imeandikwa "Karibuni wakimbizi", wakati maandamano mjini Stockholm , Helsinki na Lisbon kila mmoja yamewahusisha kiasi ya watu 1,000.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Mohammed Khelef