1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa kufanyika Venezuela

Zainab Aziz
20 Julai 2017

Wapinzani wa rais wa Venezuela Nicolas Maduro wametoa wito wa kufanyika mgomo wa kitaifa ili kushinikiza ufanyike uchaguzi wa urais na kutaka baraza maalumu litakalo pitisha katiba mpya litupiliwe mbali.

https://p.dw.com/p/2grGZ
Venezuela Krise in Caracas
Picha: picture-alliance/dpa/F. Llano

Rais wa Venezuela Nicholas Maduro na wapinzani wake leo hii wanakabiliana tena kwenye malumbano huku upinzani nchini humo ukiwa unapinga mipango ya Maduro ya kuteua baraza maalumu litakalosimamia kupatikana katiba mpya ya Venezuela.  Upinzani unasema hiyo ni njama ya rais Maduro ya kutaka kung'ang'ania madaraka. Hii leo upande wa upinzani umeitisha maandamano makubwa yanayotarajiwa kufanyika kote nchini kwa siku nzima. Maandamano kama hayo makubwa yaliwahi kufanyika nchini Venezuela mnamo mwaka 2002 lakini hayakufua dafu kumwondoa madarakani aliyekuwa rais wakati huo Hugo Chavez, na leo hii vilevile maandamano hayo yanalenga kumshinikiza rais Maduro aondoke madarakani.

Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: picture alliance/ZUMAPRESS/B. Vergara

Miaka kumi na mitano baadaye Chama kinacho tawala cha Kisoshalisti  kinadhibiti sehemu kubwa ya uchumi wa nchi hiyo jambo ambalo ni vigumu kusimamisha shughuli za kibiashara. Hata hivyo kwa upande wa upinzani jambo hilo sio kipingamizi kikubwa kwani uchumi wa Venezuela unaendelea kuzorota zaidi kutokana na kuanguka kwa bei ya mafuta na pia kukithiri kwa vitendo vya rushwa na utawala mbaya.

Kundi kubwa la wafanya biashara la Fedecamaras wakati huu halikutoa msimamo wake juu ya maandamano hayo ya leo tofauti na maandamano ya mwaka wa 2002 na yale ya mwaka 2003 ambapo kundi hilo lilishiriki katika jitihada za kutaka kumwondoa aliyekuwa rais wakati huo Hugo Chavez wakati huohuo jeshi la Venezuela limesisitiza kuwa liko tiifu kwa Rais Nicolas Maduro.  taarifa za jeshi zimesema kuwa jeshi hilo litalinda amani wakati wa kufanyika kura ya maoni yenye utata iliyoitishwa na Rais Maduro.  Raia wa venezuela wanatarajiwa kupiga kura ya maoni wiki ijayo

ambapo baraza maalumu litakaloandika katiba mpya litachaguliwa. Msimamo huo wa Jeshi wa kumuunga mkono Rais Maduro umetangazwa na Waziri wa ulinzi Jenerali Vladimir Padrino Lopez.  Hatua hiyo inalenga kupinga vitisho vya Rais wa Marekani Donald Trump vya kuiwekea Venezuela vikwazo vya kiuchumi iwapo kura hiyo itafanyika.

Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na Kanisa Katoliki vimelaani mipango ya Maduro ya kutaka kuibadili katiba ya Venezuela inayofananishwa na hatua ya kuimarisha udikteta. Maduro analaumiwa kutokana na kuzorota kwa uchumi wa taifa hilo na pia  kusababisha uhaba wa mahitaji muhimu katika taifa lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE

Mhariri: Gakuba, Daniel