1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa Togo ya kumtaka Rais ajiuzulu

Caro Robi
7 Septemba 2017

Kiongozi wa upinzani Togo amemtaka Rais Faure Gnassingbe ambaye yeye na familia yake wameiongoza nchi hiyo kwa miaka hamsini kujiuzulu maramoja akipinga hatua ya serikali ya kutaka kuibadilisha katiba

https://p.dw.com/p/2jTdr
Togo Protest #Faure Must Go
Picha: Getty Images/AFP/P. U. Ekpei

Maelfu ya waandamanaji walimiminika katika barabara za mji mkuu wa Togo, Lome wakiwa wamevalia nguo za rangi za nyekundu, chungwa na waridi, rangi za vyama vya upinzani huku maafisa wa usalama wakiwatizama. Badhi ya waandamanaji hao walibeba mabango yaliyoandikwa Togo huru na Faure jiuzulu.

Mkuu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nchini humo Aime Adi amesema zaidi ya waandamanaji laki moja walishiriki maandamano hayo ya kuishinikiza serikali kutobadilisha katiba kwa njama ya kusalia madarakani.

Familia ya Gnassingbe imekuwa madarakani miaka 50

Rais Gnassingbe ameliongoza taifa hilo la Afrika magharibi tangu baba yake afariki mwaka 2005 baada ya kuwa madarakani kwa miaka 38. Marehemu Gnassingbe Eyadema alipitisha sheria mwaka 1992 ya kuwa mihula ya kuhudumu kwa rais ni miwili pekee lakini muongo mmoja baadaye aliifutilia mbali sheria hiyo.

Belgien Togo Protest
Waandamanaji wanaipinga serikali ya TogoPicha: DW/J. C. Abalo

Baraza la mawaziri siku ya Jumanne lilidhinisha mswada wa kurejesha kikomo cha mihula ya rais lakini uamuzi huo wa baraza la mawaziri haukutuliza upinzani ambao umenoa makali.

Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa waandamanaji hao mjini Lome, Jean Pierre Fabre kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha ANC amesema wataandamana tena leo na Rais lazima awazungumzie kuhusu namna ya kuondoka madarakani.

Fabre amesema wananchi waliojitokeza kuandamana ni karibu milioni moja na kusema hakutarajia idadi kubwa kama hiyo kujitokeza kuipinga serikali. Maandamano hayo yaliitishwa na muungano wa vyama vya upinzani vya Togo.

Miji mingine pia yashuhudia maandamano

Maandamano pia yaliripotiwa katika mji wa Sokode, ulioko kaskazini mwa nchi, Dapaong, Kara  pamoja na miji mingine nchini humo. Taarifa kutoka kwa Rais imewataka wananchi kudumisha amani na utulivu na pia ameahidi kuimarisha viwango vya maisha katika taifa hilo lenye watu takriban milioni nane.

Faure Gnassingbe, Präsident Togo
Rais wa Togo Faure GnassingbePicha: AFP/Getty Images/I. Sanogo

Waziri wa utumishi wa umma Gilbert Bawara ameliambia shirika la habari la AFP kuwa serikali inazingatia kile alichokitaja matarajio makubwa ya umma na kwamba kuna kamatai inayashughulikia mapendekezo hayo huku akiwaomba wanasiasa wa upinzani kushiriki katika mazungumzo kuhusu suala la mageuzi ya katiba kuhusu muhula wa rais na mfumo wa upigaji kura.

Haijajulikana wazi ni lini mswada huo uliodhinishwa na mawaziri utawasilishwa bungeni au ni kwa kiasi gani utamuathiri Rais Gnassingbe ambaye anahudumu muhula wake wa tatu madarakani unaokamilika mwaka 2020. Bunge liko mapumziko hadi Okotoba.

Viongozi kadhaa wa Afrika wakiwemo wa Rwanda, Burundi na Burkina Faso wamejaribu kuondoa kikomo cha mihula ya rais katika miaka ya hivi karibuni ili wasalie madarakani.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Bruce Amani