1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa yaandaliwa Misri

18 Mei 2012

Chama cha Udugu wa Kiislamu kimepanga maandamano makubwa jana ya kumuunga mkono mgombea wao kwa nafasi ya Urais, Mohamed Mursi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika juma lijalo.

https://p.dw.com/p/14xRt
Mohammed Morsi , mgombea urais wa chama cha udugu wa Kiislamu
Mohammed Morsi , mgombea urais wa chama cha udugu wa KiislamuPicha: picture-alliance/dpa

Maandamano hayo kuwa katika safu ndefu kuanzia Cairo hadi Aswan wakishikana mikono umbali wa kilometa 760 ya kuomba kuungwa mkono mgombea wao na kuwashawishi wapiga kura wa Misri, taifa ambalo lipo njia panda kwa muda tangu kuondolewa madarakani kwa Rais Hosni Mubarak.

Wanachama wa chama cha Udugu wa Kiislamu cha Uhuru na haki(FJP) mitaani wakiwa na mabango yenye picha ya mgombea Mursi ambaye amekuwa mgombea mbadala baada ya mgombea wa awali wa chama hicho Khairat Shater kupigwa mkasi na tume ya uchaguzi kutokana na kuwahi kutiwa hatiani kwa makosa ya kivita.

Watakuwa katika misururu mirefu na mavazi yao yatalingana na madhari ya tukio hilo kwani watavaa fulana na kofia zenye picha ya mgombea Mursi ambaye aliwahi kuwa mhandisi hapo awali kabla ya kuingia katika siasa.

Mgombea aliyepigwa mkasi,Khairat al-Shater
Mgombea aliyepigwa mkasi, Khairat al-ShaterPicha: picture-alliance/dpa

Mabango ya Mursi mitaani

Mabango hayo yakiwa na wito wa kuwaomba wale wanaolisoma kumpigia kura Mursi wakisema Piga kura kwa Mursi kuwa Rais wa Misri. Katika mojawapo ya mtandao wa chama hicho cha udugu wa Kiislamu kumekuwa na ujumbe unaotaja kusudi lao ni kufanya maandamano yenye msururu mrefu kuomba uungwaji mkono kwa Mohamed Mursi na chama chao dunia nzima.

Chama hiki kikiwa ni miongoni mwa vyama vya siasa makini na kilichojipanga nchini humo tangu utawala wa Rais Hosni Mubarak. Sasa kinafanya kampeni kubwa za kushawishi kuungwa mkono na kupata kura za kukiwezesha kushinda uchaguzi huo.

Inaonekana wazi kuwa ushindani mkubwa upo baina ya Mohamed Mursi, Amri Moussa ambaye ni mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na mgombea wa Kiislamu Abdel Moneim Abol Fotouh.

Hamadi kibindoni

Kutokana na uimara wa Chama cha Udugu wa Kiislamu kwa muongo mmoja sasa kuna kila dalili kuweza kufanya vizuri huku kibindoni kina wabunge wengi bungeni baada ya uchaguzi wa Novemba mwaka jana.

Mojawapo ya maandamano nchini Misri
Mojawapo ya maandamano nchini MisriPicha: AP

Hali ya mafanikio hayo inaungwa mkono na Yasser Ali ambaye ni miongoni mwa watu katika safu ya kampeni ya mgombea Mohamed Mursi.

Machi mwaka huu chama cha udugu wa kiislamu kilibatilisha maamuzi yake ya kutoweka mgombea kwa nafasi ya Urais kikisema bunge ni sehemu ndogo ya kuweza kufanya maamuzi katika nchi, la msingi sasa wao lazima kushiriki kugombea Urais ili kuweza kuamua maamuzi yote muhimu ya nchi hiyo kama watashinda.

Mwandishi:Adeladius Makwega/RTRE

Mhariri: Josephat Charo