1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa yafanyika Syria

13 Aprili 2012

Maelfu ya Wasyria leo wameshiriki katika maandamano yaliyoitishwa na wapinzani wa utawala wa rais Bashar al-Assad. Kwa mujibu wa kamati ya uratibu ya kundi la wapinzani, watu watatu waliuwawa katika maandamano ya leo.

https://p.dw.com/p/14dZE
Waandamanaji Syria
Waandamanaji SyriaPicha: Reuters

Maandamano yalifanyika katika miji na vijiji vingi baada ya sala za alasiri. Kamati ya uratibu ya kundi la wapinzani imeeleza kwamba watu watatu waliuwawa leo katika maandamano yaliyofanyika katika mikoa ya Daraa, Hasakeh na Hama. Nalo shirika la kutetea haki za binadamu Syria lenye makao yake makuu mjini London, Uingereza, limeripoti kwamba maafisa wa usalama walitumia risasi kuwatanya watu waliokuwa wakiandamana baada ya sala za leo mchana.

Kulingana na taarifa za shirika hilo, maandamano yalifanyika katika mji wa Idlib ulioko kaskazini mwa Syria, katika vionga vya mji mkuu Damascus na pia katika miji ya Daraa, Homs na Latakia. Mwenyekiti wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu, Rami Abdul-Rahman, amesema kwamba kwa ujumla makubaliano ya kusitisha mapigano bado yanatekelezwa kwa sehemu kubwa, licha ya kwamba yanavunjwa kwa kiasi kidogo. Hata hivyo wanaharakati wanaeleza kwamba majeshi ya Assad yamewakamata waasi kiholela katika mji wa Daraa katika jaribio la kuwafanya waasi hao watumie nguvu dhidi ya jeshi la Assad.

Waangalizi kupelekwa Syria

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo linatarajiwa kupitisha uamuzi wa kupeleka waangalizi wa kimataifa nchini Syria. Wanadiplomasia wameeleza kwamba kundi la waangalizi 20 hadi 30 huenda likapelekwa nchini humo mwanzoni mwa wiki ijayo. Ahmad Fawzi, ambaye ni msemaji wa mjumbe maalum nchini Syria, Kofi Annan, aliwaambia waandishi wa habari kwamba kundi la wajumbe 10 hadi 12 liko tayari kwa ajili ya kutumwa kwenda Syria. Kinachosubiriwa sasa ni baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha kutumwa kwa wajumbe hao. Fawzi aliendelea kusema kuwa uamuzi wa kupeleka kundi la pili lenye hadi waangalizi 250 itabidi uainishwe pia na baraza la usalama.

Msemaji wa Kofi Annan, Ahmed Fawzi
Msemaji wa Kofi Annan, Ahmed FawziPicha: AP

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amesema hakutarajia kwamba amani ingerejea Syria kwani alikuwa na wasiwasi juu ya nia ya rais Assad. Naye Kofi Annan ameitaka Syria sasa kufungua njia ili iweze kupelekewa misaada ya kibinadamu. Wakati huo huo Uturuki imeanza kupokea misaada kutoka nje kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi wapatao 25,000 walioingia nchini humo wakitokea Syria.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFP/dpa/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman