1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria mpya unaoleta mabadiliko ya leba yazua maandamano.

John Juma15 Aprili 2016

Polisi wakabiliana na waandamanaji usiku wa Alhamisi. Waandamanaji walisababisha vurugu na kuvunja vioo vya magari na maduka. Waandamanaji hao wanapinga sheria hiyo wakisema inakandamiza haki za wafanyakazi.

https://p.dw.com/p/1IWfX
Polisi Ufaransa
Polisi UfaransaPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Mori

Kundi dogo la waandamanaji mjini Paris usiku wa Alhamisi lilifanya fujo na kuvunja madirisha ya maduka na vituo vya mabasi, hali iliyosababisha waziri wa usalama Bernard Cazeneuve kuamuru kuwa waandamanaji wanaoendeleza machafuko wakamatwe bila kuchoka.

Maandamano hayo yamesababishwa kwa sehemu kubwa na upinzani dhidi ya muswaada huo wa sheria unaozua mgawanyiko katika sekta ya wafanyakazi huku rais Francois Hollande akisema kupitia kipindi cha mjadala wa runinga kuwa sheria hiyo mpya ya leba inayopendekeza mageuzi haitaondolewa.

Mswada huo utabadili sheria zinazolinda masaa ya mtu kufanya kazi kando na kuongeza sheria nyingine kuhusu kulipwa marupurupu ya muda wa ziada kazini. Kadhalika utabadili masharti ya fidia kwa wale wanaoachishwa kazi bila haki kuzingatiwa huku ukilenga sheria zinazolinda vyama vya wafanyakazi.

Waandamanaji wasababisha uharibifu

Kundi la waandamanaji lililenga afisi ya ajira, maduka makuu na kituo cha magari. Maandamano ya amani yamekuwepo kwa wiki kadhaa nchini Ufaransa kuipinga sheria hiyo iliyowasilishwa na waziri wa leba Myriam El Khomri. Sheria inayotizamwa kama ya ukandamizaji wa haki za wafanyakazi zilizopatikana kwa dhiki mfano kufanya kazi kwa muda wa saa 35 kila wiki.

Waziri wa usalama Bernard Cazeneuve
Waziri wa usalama Bernard cazeneuvePicha: picture-alliance/AP Photo/G. Vanden Wijngaert

Akikosoa vurugu za maandamano ya Alhamisi usiku, ambayo ameyataja kuwa ni kitendo kisichokubalika Cazeneuve alisema “ wale wasiokuwa na maadili na wanaoongozwa tu na hisia za kuzua ghasia watasakwa na kukamatwa na vikosi vya polisi.

Maandamano hayo pia yalizua makabiliano kati ya polisi na vijana, ambapo polisi walitumia gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji. Waziri Cazeneuve alinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema polisi 151 walijeruhiwa kwenye maandamano hayo.

Mwandishi: John Juma/DPAE/RTRE

Mhariri: Yusuf Saumu