1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya Iran na umri wa wakimbizi Magazetini

Oumilkheir Hamidou
3 Januari 2018

Maandamano nchini Iran, majadiliano ya kuundwa serikali ya muungano Ujerumani na mjadala kama umri wanaotoa wakimbizi ni wa kweli au wa hadaa ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/2qGJs
Iran, Teheran, Protest
Picha: Getty Images

Tunaanzia Iran ambako vijana wanaendelea kuteremka majiani kulalamika dhidi ya shida za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Viongozi wa kidini wanawatuhumu mashawishi kutoka nje kuwa nyuma ya maandamano ya umma. Gazeti la "Der neue Tag" linaandika: "Ni kawaida: wananchi wanapoteremka majiani wakilalamika dhidi ya viongozi wao, daima wageni ndio wanaonyooshewa kidole cha lawama . Ni jambo lililokuwa likitarajiwa kwa hivyo kumuona Ayatollah Ali Khamenei akitoa maneno yasiyo ya upole, kama yale yaliyotolewa na rais wa Iran Hassan Ruhani. Katika wakati ambapo rais Ruhani anaonyesha kukielewa kilio cha waandamanaji, kiongozi wa kidini wa jamhuri ya kiislam anahisi "maadui wa Iran" ndio wanaopalilia maandamano hayo. Hatima ya utawala  uliodhoofika wa Teheran inakurubia. Suala ni kama madaraka ya wafuasi wa itikadi kali yatadhoofika pia na kama ndio , basi lini?"

Picha za Ayatollah Ali Khamenei zatiwa amoto Teheran

 Gazeti la kaskazini mwa Ujerumani "Hannoversche Allgemeine" pia lina maoni kama hayo kuhusiana na tuhuma za viongozi wa Iran dhidi ya ushawishi kutoka ng'ambo. Gazeti linaandika: "Mamullah wao wanaona, hakuna chengine kinachosababisha maandamano katika sehemu kubwa ya nchi yao ila ushawishi kutoka nje. Kidole wananyooshewa maadui wa jadi, Saud Arabia. Ukweli lakini ni kwamba ghadhabu za wananchi wenyewe ndizo zinazoutikisa utawala katika jamhuri hiyo ya kiislam. Wimbi hili jipya la maandamano lina nguvu zaidi kuliko lile la mwaka 2009. Na jazba pia ni kubwa. Kwa mara ya kwanza kabisa picha za kiongozi wa kidini, Ayatollah Ali Khamenei zimetiwa moto mjini Teheran."

Mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano mjini Berlin

Mada yetu ya pili magazetini inatupeleka Berlin ambako mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikuu, CDU/CSU na SPD yanatarajiwa kuanza january saba inayokuja. Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linazungumzia vizingiti vinavyowekwa hata kabla ya mazungumzo kuanza. Gazeti linaendelea kuandika: "CSU wanatoa masharti ya kila aina hata kabla ya mazungumzo pamoja na SPD kuanza. Mazungumzo hayatakua rahisi kwa hivyo. SPD wameshawaahidi wafuasi wao mashinani, watajadiliana bila ya kulenga matokeo maalum. Na hiyo sio mbinu wala njama za kisiasa bali ni suala la uaminifu. Kwa hivyo wakuu wa vyama ndugu vya CDU/CSU watalazimika kuridhia mengi ikiwa watataka kuendeleza serikali ya muungano wa vyama vikuu pamoja na SPD."

Umri wa waakimbizi wawekewa suala la kuuliza

Mada yetu ya mwisho magazetini inazungumzia mjadala ulioenea humu nchini kama wakimbizi vijana wanaoingia humu nchini wachunguzwe kama umri wanaootoa kujisajili kama wakimbizi ni wa kweli au wa hadaa. Gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" linaandika: "Sasa kwa hivyo wanataka kulazimisha uchunguzi wa kitabibu ufanywe kwa wote wale wanaojitaja kuwa wakimbizi vijana. Vyama ndugu vya CDU/CSU havijakosea, watu wasikubali, wahamiaji wanaopo toa umri mdogo kwa lengo la kukwepa kuhukumiwa  au kwa lengo la kupewa adhabu hafifu. Au hata kujiimarishia fursa ya kukubaliwa kuishi humu nchini kama mkimbizi. Hata hivyo kivitendo madai kama hayo hayana maana; kwasababu hayamzuwii mkimbizi kufanya uhalifu. Na sio hayo tuu, utaratibu wenyewe wa kuchunguza umri wa kweli unaweza kuangaliwa kua kinyume na haki za binaadam.

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman