1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano dhidi ya SGR yafanyika Mombasa

Amina Mjahid
4 Oktoba 2019

Wafanyabiashara wa kampuni za kibinafsi za shughuli za uchukuzi bandarini Mombasa, wamepinga amri ya wizara ya kusimamisha kwa muda agizo linalolazimisha makasha ya mizigo inayoingia bandarini Mombasa kubebewa na SGR

https://p.dw.com/p/3Qj6H
Mombasa
Picha: DW/F. Musa

Wafanyabiashara hao mbali mbali wakiongozwa na mwenyekiti wa vuguvugu la jamii ya wafanyabiashara la Fast Action, Salim Karama, wamesema hawakuhusishwa katika kikao cha maamuzi hayo na vile vile tangazo la waziri halikujali waliofutwa kazi sawa na kwamba agizo linalolazimisha mizigo kubebwa na SGR sio sheria bali maamuzi ya mamlaka ya ukusanyaji ushuru na mamlaka ya bandari.

Katibu Mtendaji katika vuguvugu hilo Harriet Muganda amewakana viongozi wa Mombasa waliohudhuria kikao hicho kilichotoa tamko la kusimamishwa kwa muda kwa uchukuzi wa mizigo kupitia SGR, akieleza kwamba viongozi hao walioongozwa na gavana Hassan Joho sio wakilishi wa wafanyabiashara na wala hawana ukweli katika kuwatetea watu wa Mombasa juu ya swala la SGR.

Mipango maalum inayojumuisha kila mtu katika sekta ya uchukuzi inahitajika

Mombasa
Wafanyabiashara na wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu waandamana kupinga agizo la mizigo yanayowasili bandarini kupelekwa mjini Nairibi kupitia SGR Picha: DW/F. Musa

Wafanyabishara hao wameshikilia kuendelea na maandamano yao ya kila Jumatatu ya wiki sawa na kukongamana katika uwanja wa Tononoka siku ya sherehe ya kitaifa ya Mashujaa, Oktoba 20, ambapo rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ataongoza sherehe hiyo katika bustani la Mama Ngina mjini Mombasa.

Hapo jana waziri wa uchukuzi James Macharia akiwa na viongozi wa Mombasa alisema agizo hilo liliwahi kusimamishwa miezi kadhaa na kwamba hadi sasa wanasisitiza kusimamishwa kwake, japo wafanyabiashara wanasema jambo hilo halitekelezwi kwa sababu uchukuzi wa mizigo unaendelea.

Gavana wa Mombasa ameitaka wizara ya uchukuzi kuweka mipango maalum inayojumuisha kila mdau katika sekta ya uchukuzi kuhakikisha uchukuzi wa mizigo kupitia reli ya kisasa unafanyika kwa njia ya kumfaa kila mfanyabiashara, kuinua uchumi wa Mombasa na wa mkaazi wa Mombasa. 

Chanzo: Faiz Musa