1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya siku mbili yaanza Venezuela

Sylvia Mwehozi
26 Julai 2017

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Leopoldo Lopez ametoa ujumbe wake wa kwanza tangu aachiliwe kutoka kifungo cha nyumbani mwezi huu wakati ambapo mgomo wa nchi nzima wa siku mbili ukianza siku ya Jumatano. 

https://p.dw.com/p/2hBmG
Venezuela Caracas Proteste
Picha: picture-alliance/AA/C. Becerra

Kiongozi huyo amewataka Wavenezuela wote kuunga mkono mgomo wa masaa 48 ulioanza leo jumatano, kupinga mipango ya serikali ya kuandika upya katiba na kuliomba jeshi kutokandamiza maandamano. Katika ujumbe wa mkanda wa video uliorekodiwa nyumbani kwake na kutolewa usiku wa kuamkia leo, Lopez anasema utawala wa rais Nicolas Maduro unatafuta kuharibu kabisa demokrasia. Ametoa wito kwa Wavenezuela kuzuia mipango hiyo kwa  upinzani wa Amani.

"Ninawaambieni kwamba, kama imani yangu, mapambano yangu na dhamira yangu ya kuwasindikiza watu wa Venezeula kwamba kwa pamoja tutashinda demokrasia, kama hii inawakilisha hatari ya mimi kurejeshwa jela! niko tayari kuingia katika hatari hiyo," amesema Lopez.

Venezuela Freilassung von Leopoldo López, Oppositionsführer
Kiongozi wa upinzani Venezuela Leopoldo López Picha: Getty Images/AFP/J. Hernandez

Mgomo wa nchi zima wa siku mbili ni jaribio la mwisho la kumshinikiza rais Maduro kuachana na uchaguzi uliopangwa kufanyika mwishoni mwa juma wa kuliteua bunge maalumu ambalo wapinzani wanasema litahalalisha utawala wa mtu mmoja.

Majirani walikusanyika katika miji ya Venezeula wakizuia barabara kwa takataka, mawe na utepe, wakati migahawa mingi na biashara ikisalia imefungwa katika maandamano ya kupinga dhamira ya chama tawala cha kisosholisti ya kufanya kura ya bunge iliyopangwa.

Kulikuwa na shauku kidogo ya maandamano, hata hivyo kwa tabaka la wafanyakazi na maeneo ya vijijini ambako serikali kijadi imekuwa ikitoa msaada zaidi.

Kwa ujumla ni idadi ndogo ya watu waliotilia umakini maandamano hayo ukilinganisha na umati uliojitokeza katika maandamano ya masaa 24 yaliyofanyika wiki iliyopita. Jose Vicente Rangel Avalos ni mmoja wa wagombea katika bunge la katiba, "tutawaonyesha upinzani kwamba nchi yetu kubwa na uchaguzi tutakaofanya, utakuwa ni pigo machoni kwa wachache ambao wanataka vurugu na uharibifu."

Venezuela Kolumbien Migration
Wavenezuela wakivuka mpaka na kuingia Colombia kununua bidhaa muhimuPicha: Getty Images/AFP/L. Acosta

Wavenezuela wengi bila kujali mitazamo yao ya kisiasa, walikuwa na wasiwasi juu ya athari za kifedha katika mifuko yao na chakula. Taifa hilo la muungano wa nchi zinazouza mafuta duniani OPEC,  limetumbukia katika mgogoro mbaya wa kiuchumi, likikabiliwa na uhaba wa bidhaa za msingi kama chakula na madawa.

Rais Maduro mwenye miaka 54 ambaye anajiita mtoto wa Chaves na mpeperusha bendera ya ujamaa katika karne ya 21, amesisitiza kwamba kura ya Jumapili itaendelea kama ilivyopangwa licha ya shinikizo kali kutoka ndani na nje ikiwemo vitisho vya kiuchumi kutoka kwa Marekani.

Anasema bunge la katiba lenye viti 545,  litakuwa na mamlaka ya kuiandika upya katiba ya nchi na kupiku maamuzi ya bunge linaloongozwa na upinzani na kwamba limepangwa kuelekeza mamlaka mikononi mwa wananchi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga