1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yatawala siku ya wafanyakazi

Admin.WagnerD1 Mei 2014

Polisi nchini Uturuki imetumia nguvu kuwatanya waandamanaji wa siku ya wafanyakazi duniani leo, wakati maelfu kwa maelfu wakiingia mitaani duniani kote kuadhimisha siku hiyo maarufu kama Mei Dei.

https://p.dw.com/p/1BrwN
Waandamanaji nchini Uturuki wakikabiliana na polisi mjini Istanbul.
Waandamanaji nchini Uturuki wakikabiliana na polisi mjini Istanbul.Picha: Reuters

Katika mji uliyoshupana wa Instabul, polisi imewatawanya mamia ya waandamanaji waliojaribu kukaidi marufuku ya kuandamana katika uwanja wa Taksim mjini humo, katika kumbukumbu ya makabailiano yaliyozaa vuguvugu la kitaifa la maandamano.

Baada ya kutoa onyo la mwisho, polisi wa kuzuwia ghasia wakisaidiwa na magari ya maji ya kuwasha waliwakabili waandamanaji katika wilaya ya Besiktas wakati wakijaribu kuvunja vizuwizi vilivyowekwa kuelekea uwanja huo.

Mikutano imefanyika barani Asia kote, ikiwemo katika miji ya Hong Kong, Jakarta, Kuala Lumpur, Singapore, Taipei na Seoul, ambako maandamano ya kila mwaka yalitarajiwa kughubikwa na maafa yaliyosababishwa na ajali ya feri hivi karibuni.

Mjini Moscow, limefanyika gwaride kwa mara ya kwanza tangu ulipovunjika muungano wa Kisoviet mwaka 1991.
Mjini Moscow, limefanyika gwaride kwa mara ya kwanza tangu ulipovunjika muungano wa Kisoviet mwaka 1991.Picha: REUTERS

Gwaride larejeshwa Urusi

Wakati huo huo, wafanyakazi nchini Urusi walifanya gwaride katika uwanja mwekundu mjini Moscow kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1991 - huu ukiwa utamaduni wa hivi karibuni wa zama za muungano wa kisovieti kuhuishwa wakati ambapo wimbi la uzalendo likizidi kukita mizizi nchini humo.

Mei Dei ilikuwa siku muhimu katika kalenda ya kisovieti, ikiadhimishwa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo magwaride ya wanariadha, wanajeshi na wafanyakazi katika uwanja wa umma mjini Moscow, lakini katika siku za hivi karibuni, maandamano hayo ya kila mwaka yalikuwa yakifanyika tu katika barabara kuu ya mji huo.

Nchini Cambodia, vikosi vya usalama vilivyojihami kwa bakora na virungu viliwatawanya kwa nguvu waandamanaji kadhaa karibu na uwanja wa uhuru mjini Phnom Penh, ambako mpiga picha wa shirika la habari la AFP alishuhudia watu kadhaa wakipigwa.

Polisi ya Indonesia ilisema wafanyakazi wapatao 30,000 walipanga kuandamana mjini Jakarta. Vyama vya wafanyakazi vilisema hadi wafanyakazi milioni mbili wangejitokeza kudai mazingira bora ya kazi katika taifa hilo lenye wakaazi wengi zaidi kusini-mashariki mwa Asia, ingawa katika miaka ya nyuma idadi ya waandamanaji imekuwa chini sana kuliko ile inayobashiriwa na vyama hivyo.

Maandamano mjini Los Angeles.
Maandamano mjini Los Angeles.Picha: Kevork Djansezian/Getty Images

Mjini Hong Kong, waandaji walisema watu 5,000 walitarajiwa kujiunga na maandamano yao kutoka bustani ya Victoria hadi makao makuu ya serikali, huku suala la kipaumbele kwenye ajenda yao likiwa masaa bora ya kufanya kazi.

Ajali ya feri yaghubika Korea Kusini

Makundi ya kiraia nchini Malaysia, yalisema yalitarajia maelfu kadhaa kuhudhuria mkutano wa hadhara mjini Kuala Lumpur kupinga ongezeko la bei za bidhaa lililotekelezwa na serikali ya muda mrefu ya nchi hiyo, ambayo tayari inamulikwa ndani na nje ya nchi kutokana na namna ilivyoshughulikia kupotea kwa ndege ya abiria Machi 8.

Mjini Seoul, karibu wafanyakazi 5,000 walitarajiwa kukusanyika nje ya kituo cha reli cha Seoul mchana, lakini mkusanyiko wa mwaka huu umeghubikwa na janga la kivuko kilichogharimu maisha ya mamia ya watu, wengi wao wakiwa wanafunzi wa shule.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre,dpae
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman