1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yavuruga biashara na uchumi wa Hong Kong

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
18 Septemba 2019

Maandamano ya Hong kong ambayo yameendelea kwa miezi minne yamesababisha hasara kubwa hasa kwenye sekta ya utalii. Wafanyabiashara kwenye jiji hilo wamelazimika kupunguza idadi ya wafanyakazi wao.

https://p.dw.com/p/3PoMM
Vladdo Karrikatur Alerta máxima

Ghasia katika mji huo wa Hong Kong zimesababisha wasafiri wengi kukiepuka kisiwa hicho ambacho ni kitovu cha masuala ya biashara na fedha. Na kutokana na kutokuwepo na dalili zozote za waandamanaji na serikali za kurudi nyuma, kuna wasiwasi mkubwa kwamba hali haitatokuwa shwari hivi karibuni.

Idadi ya wageni kutoka China Bara imepungua baada ya lawama za wazi kwa waandamanaji kutoka Beijing, ambayo imeyafananisha machafuko hayo na vitendo vya ugaidi. Msemaji wa baraza la viwanda na safari la Hong Kong, Jessica Wan ameliambia shirika la AFP kwamba  idadi hiyo ya watalii kutoka China Bara ilipungua kwa asilimia 90 katika siku 10 za kwanza za mwezi huu Septemba.

Wakati huo huo shirika la ndege la Hong Kong Cathay Pacific limeripoti pia kushuka kwa idadi ya abiria kwa asilimia 11 katika mwezi wa Agosti, wakati maeneo mawili kwenye uwanja wa ndege yalipozuiwa na waandamanaji na kusababisha kufutwa kwa mamia ya safari za ndege.

katika mwezi wa Agosti kulishuhudiwa kuporomoka kwa kiwango kikubwa cha wageni kuliko hata wakati lilipotokea janga la virusi vya maambukizi ya mfumo wa kupumua, SARS mnamo mwaka 2003 ambapo karibu watu 300 walipoteza maisha.

Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam
Kiongozi wa Hong Kong Carrie LamPicha: Reuters/A.A. Dalsh

Mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na vurumai za maandamano hayo ni eneo la Causeway Bay la biashara ya bidhaa za kifahari ambapo wauzaji wa maduka na wateja mwishoni mwa wiki iliyopita walijikuta kwenye wakati mgumu pale polisi walipotumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya vijana wanaoandamana mjini Hong Kong. Mfamasia mmoja katika kitongoji hicho, ambaye alijitaja kwa jina moja tu Chiu, aliwaambia waandishi wa habari wa AFP kwamba mauzo yamepungua mno tangu maandamano yalipoanza mnamo mwezi Juni.

Ameongeza kusema kwamaba mazingira sio mazuri na mara kadhaa amelazimika kufunga duka lake hali inayosabisha biashara yake kushuka kwa asilimia 40 hadi 50. Amesema wateja hawanunui sana na hivyo biashara yake inaendelea kuwa mbaya kuliko wakati zilipofanyika harakati za mwavuli za mwaka 2014.

Mzozo wa Hong Kong wa muda mrefu umeambatana na kuzorota kwa sekta ya uagizaji na uuzaji nje duniani kote pamoja na vita ya biashara kati ya Marekani na China. Mapema mwezi huu kampuni ya Fitch iliiteremshia Hong Kong kiwango cha hadhi ya jiji lake kutokana na maandamano hayo.

Chanzo:/AFP