1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano Yemen yakamilika

3 Februari 2011

Maelfu ya waandamanaji wameshiriki katika maandamano yaliopewa jina 'siku ya hasira', katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a, hii leo, yaliokwisha kwa amani.

https://p.dw.com/p/10ALL
Waandamanaji wanapinga serikali ya rais Ali Abdulla SalehPicha: dapd

Hatahivyo polisi walilazimika kufyatua hewa ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika mji wa Aden, kusini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, zaidi ya watu 20,000 wanaomuunga mkono rais Ali Abdulla Saleh waliandamana karibu na chuo kikuu cha Sana'a, huku kundi linaloipinga serikali likikusanyika katika eneo la al-Tahrir.

Wakati huo huo, waandamanaji zaidi ya 20,000 wanaoipinga serikali na walioitisha maandamano ya 'siku ya hasira',walitembea kutoka kitongoji cha Bab al -Yemen, kilicho umbali wa kilomita nne kutoka mji wa Sana'a.

Lakini pande zote zilirudi nyumbani mchana wa leo pasi na kutokea vurugu zozote mjini humo.

Vurugu mjini Aden

Proteste im Jemen
Picha: dapd

Ama kwa upande wa mji wa bandari uliopo kusini mwa nchi hiyo, Aden, mashahidi wanasema maafisa wa polisi walifyatua hewa ya kutoa machozi na risasi ili kuwatawanya waandamanaji wanaoipinga serikali na kuwajeruhi watu wawili.

Kwa mujibu wa mwandishi mmoja wa shirika la habari la AFP, maafisa wa polisi walienea kwa wingi mapema leo asubuhi na kuwatawanya waandamanaji hao walipoanza kutembea mjini humo.

Maandamano hayo, yakiwa ni sehemu ya yale yaliofanyika mjini Sana'a ya 'siku ya hasira' , yaliandaliwa na muungano wa upinzani ujulikanao kama Common Forum dhidi ya utawala wa rais Saleh.

Mamia ya waandamanaji walikusanyika, wengine wakibeba mabango yalio na ujumbe, 'wafisadi na madikteta ni lazime waondoke', na 'wakati wa mabadiliko umefika.'

Katika sehemu nyengine ya mji huo polisi iliwakamata watu 30 waliojaribu kuanzisha maandamano yanayofanyika kila siku ya Alhamisi kutaka kuachiwa wafungwa, maafisa wanaounga mkono uhuru wa eneo la kusni mwa nchi hiyo.

Proteste im Jemen
Picha: AP

Maelfu ya watu waliandamana pia katika miji mbalimbali ya eneo hilo la kusini, wengine ikiwa ni kuitikia wito wa kujitenga eneo hilo, huku wengine kufuatia ombi la Common Forum kuipinga serikali ya nchini humo.

Utawala wa rais Saleh

Hapo jana rais Saleh, aliyeiongoza nchi hiyo tangu 1978, aliahidi hatogombea tena kuchaguliwa ifikapo mwaka 2013 wakati muhula wake utakapokwisha, na pia kuwa hatomwachia mwanawe wadhifa huo.

Amesema uchaguzi wa bunge wa mwezi Aprili utaahirishwa, wakati rais na chama tawala wanajaribu kuunda serikali ya umoja wa taifa na upinzani.

Yemen ina mizozo tofauti ya ndani, likiwemo azimio la kujitenga kwa maeneo ya kusini kutoka kaskazini, na tishio la kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika eneo la Bara Arabu

Nchi hiyo pia ni maskini zaidi katika eneo hilo la Ghuba, ambapo zaidi ya nusu ya wakaazi wake milioni 23 wanaishi katika umaskini.

Mwandishi Maryam Abdalla/Dpae/Afpe
Mhariri: Miraji Othman