1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko Baraza la Mawaziri Tanzania

23 Machi 2017

Rais John Magufulli amemteua Harrison Mwakyembe, aliyekuwa Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba, kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Sanaa, nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Nape Nnauye.

https://p.dw.com/p/2Znq2
Nape Nnauye
Picha: DW/YTalib

Nafasi ya Mwakyembe inajazwa na Profesa Paramagamba Kabudi. Hatua hii imekuja katika wakati ambapo kumekuweko na wasiwasi kwamba huenda waziri Nape Nnauye angejiuzulu baada ya kuibuka kile kinachoonekana kuwa mvutano kati yake na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliyevamia kituo cha matangazo ya redio na televisheni  cha Clouds akiwa na kundi la maofisa wa polisi. Mengi yanazungumzwa kuhusiana na hatua hiyo ya ghafla iliyochukuliwa na rais Magufuli  ambapo taarifa ya mabadiliko hayo haikulitaja kabisa jina la Bwana Nnauye. 

Nnauye alifanya mkutano na waandishi wa habari akiwaomba wananchi wa Tanzania wamuunge mkono waziri aliyechukua nafasi yake, Harrison Mwakyembe na pia Rais John Magufuli. Amesema pia mambo yako sawa, akiwataka watu watulie na kusisitiza kuwa huu si wakati kuvuruga nchi yetu. Ameahidi pia kuendelea kuwatumikia wananchi kama mbunge. 

Nape Nnauye azungumza na wanahabari

Kulitokea mvutano mkubwa baina ya Nape Nnauye na maofisa wa polisi waliokuwa wakijaribu kumzuia mwanasiasa huyo kutozungumza na waandishi wa habari kuelezea msimamo wake baada ya kuvuliwa wadhifa huo na Rais John Magufuli. 

Mvutano huo uliodumu kwa saa kadhaa ulizuka baada ya mwanasiasa huyo kuwasili katika eneo ambalo alipanga kukutana na waandishi wa habari. Gari lake likiwa na namba za Serikali lilizongwa mara moja na polisi walimzuia kushuka wakitaka aondoke. Huku akipinga kuondolewa kwa nguvu kwenye eneo hilo, Nape alilazimika kuliegemea gari lake na ghafla alishuhudiwa askari moja aliyekuwa amevalia kirai akitoa bastola kumtisha mbunge huyo wa Jimbo la Mtama. 

Hali ilikuwa ni ya mshike mshike kwenye eneo hilo na ndipo mbunge huyo aliamua kupanda juu ya gari na kuhoji kubinywa uhuru wake wa kutoa maoni. Alisema kamwe hatanyamaza kusema ukweli hasa kwa vile amefunzwa na waasisi wa taifa hili kupigania haki na kweli na akawaka vijana kutembea kifua mbele kutoingia na hofu juu ya jambo lolote kwa vile wapo katika taifa lao lililo huru. Alisema anashangazwa kuona leo anazuiliwa kutozungumza na waandishi wa habari ili hali ndiye aliyepigana kufa na kupona katika uchaguzi uliopita kuhakikisha CCM inasalia madarakani. 

Akizungumzia kuhusu kuvuliwa madaraka na Rais Magufuli, mbunge huyo alisema amepokea uamuzi huo kwa mikono miwili na kwamba ataendelea kuiunga mkono serikali iliyopo madarakani. Kuondolewa kwa Nape kwenye wadhifa wake kumekuja siku moja baada ya kukabidhiwa ripoti iliyoelezea uvamizi uliofanywa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam katika chombo cha habari cha Clouds. Nape anaungana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Charles Kitwanga kuwa mawaziri waliodumu kwa muda mfupi katika utawala wa Rais Magufuli.