1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko yaendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati licha ya kuwepo serikali mpya

Admin.WagnerD27 Januari 2014

Hali katika Jamhuri ya Afrika kati bado ni tete.Kiasi ya watu wanane wameuawa katika mji mkuu Bangui na maafisa wakuu wa kundi la waasi la Seleka wameripotiwa kuutoroka mji huo

https://p.dw.com/p/1Axfr
Picha: E.Feferberg/AFP/GettyImages

Milio ya risasi ilisika usiku kucha katika eneo la Miskine viungani mwa mji mkuu Bangui ambako kunashikwa doria na wanajeshi kutoka kikosi cha umoja wa Afrika MISCA wakisaidiwa na wanajeshi wa Ufaransa.

Kiasi ya watu milioni moja au robo ya idadi ya raia wa Jamhuri ya Afrika ya kati wameachwa bila makaazi tangu mapigano yalipoanza mwezi machi mwaka jana kati ya waasi wa kiislamu wa Seleka na kundi la waasi wa kikiristo wajiitao anti Balaka.

Watu zaidi waendelea kuuawa

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 2,000 wameuawa katika machafuko hayo ya kulipiza kisasi kati ya makundi hayo mawili ya kidini licha ya majeshi ya Ufaransa na ya Umoja wa Afrika kwenda nchini humo ili kurejesha hali ya utulivu na kusitisha umwagaji wa damu.

Waasi wa kundi la Seleka mjini Bangui
Waasi wa kundi la Seleka mjini BanguiPicha: Reuters

Mkuu wa shirika la msalaba mwekundu nchini humo Antonie Mbao Bogo amesema mauaji ya hapo jana yalikuwa mabaya, kwani waathiriwa walichinjwa kama wanyama kwa mapanga huku wengine wakiachwa na majeraha.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameonya kuwa nchi yake inajitayrisha kuwawekea vikwazo wale wote wanaohusika na mapigano hayo ya kikabila.

Kerry ameongeza kuwa ili ghasia hizo ziache kuzagaa na kusababisha mauaji zaidi,viongozi wa Jamhuri ya Afrika ya kati wa sasa na wa zamani sharti waweke bayana kuwa wanalaani vitendo hivyo.

Marekani imeahidi msaada wa takriban dola milioni 101 kusimamia usafiri,vifaa,mafunzo na masuala ya kiufundi kwa jeshi la kikosi cha MISCA.

Viongozi wa Seleka watoroka Bangui

Haijabainika wazi ni kwanini viongozi wa waasi wa Seleka waliokuwa wakisafiri kwa msafara wa magari zaidi ya ishirini wkisindikizwa na majeshi ya Chad,waliondoka Bangui na walikuwa wakielekea wapi.

Rais mpya wa mpito wa nchi hiyo Catherine Samba Panza aliyeapishwa Alhamisi iliyopita ameahidi kufanya mazungumzo na makundi hayo ya waasi ili kujaribu kurejesha hali ya utulivu.

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba Panza
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba PanzaPicha: Reuters

Waziri mkuu mpya wa taifa hilo Andre Nzapayeke aliyechaguliwa siku ya Jumamosi na Rais Samba Panza pia amesema atakutana na pande zote mbili kutafuta suluhu ya kukomesha mapigano.

Hapo jana shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International lilionya kuwa kuna hofu kutatokea mauaji ya kiwango kikubwa katika miji ya kaskazini magharibi ya Baoro na Bossemptle ambako raia na nyumba zao walichomwa wiki iliyopita.

Utawala mpya wa Bi Samba Panza una kibarua kigumu mbele yake ya kuunda serikali kamili,kukomesha mapigano na kuliunganisha taifa hilo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman