1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machar, Kiir wasaini muafaka mpya

John Juma
6 Agosti 2018

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake mkuu, Riek Machar, wamesaini makubaliano ya kugawana madaraka katika hatua inayolenga kurejesha amani baada ya vita vikubwa vilivyouwa maelfu ya watu.

https://p.dw.com/p/32fhJ
Sudan Khartum Abkommen zur Machtteilung im Südsudan unterzeichnet
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Mahasimu hao wawili walisaini makubaliano hayo jana Jumapili (Agosti 5) katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, mbele ya mwenyeji wao, Rais Omar Hassan al Bashir na marais wenzake kutoka Kenya, Uganda na Djibouti pamoja na wanadiplomasia wa kigeni.

Mara tu baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo yanayofungua njia kwa mkataba wa amani unaolenga kumaliza vita katika taifa hilo changa kabisa, Rais Kiir alisema ni sharti yatoe mwelekeo wa kumaliza vita, huku akiwataka viongozi wote kuyazingatia.

"Lazima tuwe wakweli na tukubali kwamba vita vya ndani, ambavyo tumejihusisha navyo kama Wasudan Kusini kwa miaka mitano iliyopita, havina maana kabisa. Vimewapa raia wetu mateso makali, na kusababisha vifo visivyokuwa na maana kwa mamia ya vijana, waume na wanawake. Vimeharibu uchumi wetu na kuacha nchi yetu ikiwa imegawika zaidi ya hapo awali."

Kwa upande wake, alisema mkataba huo ni wa kushangiriwa sio Sudan Kusini pekee bali kwa ulimwengu mzima, huku akiihimiza Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) inayozisimamia juhudi za hivi karibuni za kutafuta amani kwa Sudan Kusini, kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa. 

"Wakati mwingine shetani huwa katika utekelezaji. Ikiwa hakuna nia ya kisiasa, hata tukisaini makubaliano yanayopendeza lakini hayajatekelezwa, hatutakuwa tumefanya kitu."

Mgawanyo wa madaraka

Uganda Südsudan - Friedensgespräch zwischen Präsident Kiir, Oppositionsführer Machar und der ugandische Präsident Museveni
Salva Kiir (kulia) na hasimu wake mkuu Riek Machar (kushoto) wakiwa chini ya upatanishi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: Getty Images/AFP/S. Sadurni

Chini ya makubaliano hayo, kutakuwa na mawaziri 35 kwa serikali ya mpito, 20 wakitoka upande wa Kiir, tisa kutoka kundi la Machar na wengine wakiwakilisha makundi mengine ya waasi. 

Bunge litakuwa na wajumbe 550, ambapo 332 watatoka upande wa Kiir na 128 kutoka kundi la Machar.

Hata hivyo, Kiir alionya kuwa serikali kubwa itasababisha changamoto. 

Baada ya mkataba wa mwisho wa amani kusainiwa, mahasimu hao wawili watakuwa na miezi mitatu kuunda serikali ya mpito ambayo itakaa madarakani kwa miaka mitatu. 

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan na kujipatia uhuru mwaka 2011, lakini vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka miaka miwili baadaye kati ya serikali inayoongozwa na Kiir na vuguvugu la waasi lililoongozwa na Machar. 

Vita hivyo vilivyochochewa na uhasama wa kibinafsi kati ya Kiir na Machar vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kulazimisha robo ya raia milioni 12 wa nchi hiyo kuyakimbia makaazi yao, huku vikiulemaza uchumi ambao unategemea pakubwa uzalishaji wa mafuta. 

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa mahasimu hawa kuweka saini makubaliano ya amani. Mikataba ya amani ya awali ilidumu kwa miezi michache tu kabla ya vita kuzuka tena.

Na hata kwa huu wa sasa, baadhi ya wachambuzi wameibua maswali ikiwa mkataba wa sasa utadumu.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga