1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua ya kusimamishwa mapigano nchini Syria yasubiliwa

Isaac Gamba26 Februari 2016

Rais Barack Obama wa Marekani amezitahadharisha Urusi na Syria kuwa dunia itakuwa inatizama kusubiri utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa ya kusimamisha mapigano nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1I2mD
Zana za kivita za Urusi nchini Syria
Zana za kivita za Urusi nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP

Rais Obama amesema siku zinazofuatia zitakuwa muhimu sana kufuatia makubaliano yaliyofikiwa baina ya Marekani na Urusi juu ya kusimamisha vita ambavyo vimekuwa vikiendelea nchini Syria, ambayo pia yameungwa mkono na utawala wa Rais Bashar al- Assad pamoja na makundi ya upinzani nchini humo. Hatua hiyo ya kusimamisha mapigano ambayo hailihusu kundi la Dola la kiisilamu pamoja na makundi mengine ya itikadi kali, inaonekana kuwa hatua moja kubwa ya jitihada za kidiplomasia za kusaidia kumaliza mzozo huo wa Syria, licha ya kuwepo na mashaka ya kufanikiwa kwa utekelezaji wake kutokana na kukwama kwa juhudi za awali za aina hiyo.

Wajumbe kutoka mataifa 17 yanayounga mkono mpango huo wanatarajiwa kukutana hii leo mjini Geneva kukamilisha masuala kadhaa yanayohusiana na makubaliano hayo.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia makubaliano juu ya hatua hiyo yanatarajiwa pia kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia hii leo.

Kuna matumaini kuwa mafanikio ya hatua hiyo yatasaidia kufufua mazungumzo ya amani ambayo yalivunjika mjini Geneva mapema mwezi uliopita.

" Kesho itakuwa ni siku muhimu sana, nasema ni siku muhimu sana" amesema mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na mgogoro huo wa Syria Staffan de Mistura, akizunguza na waandishi wa habari hapo jana mjini Geneva. Hata hivyo makubaliano hayo yanaruhusu kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya kundi la (IS) ambalo linadhibiti maeneo makubwa nchini Syria pamoja na Iraq tangu mwaka 2014 pamoja na makundi mengine ya itikadi kali likiwemo kundi la Al-Nusra Front lenye mahusiano na kundi la Al-Qaeda.

Marekani yadai kuanza kufanikiwa katika kulidhibiti Dola la Kiisilamu

Rais Barack Obama.alisema anaamini kuwa makundi hayo ya itikadi kali yataendelea na mashambulizi lakini bado akasisitiza kuwa mashambulizi yanayoongozwa na Marekani na washirika wake yalikuwa yanaonekana kupata mafanikio katika kulidhibiti kundi hilo.

Rais Barack Obama akizungumza juu ya mgogoro wa Syria
Rais Barack Obama akizungumza juu ya mgogoro wa SyriaPicha: Reuters/C. Barria

Kwa upande wake Rais wa Urusi Vladmir Putin ameahidi kufanya kila atakaloweza kuhakikisha makubaliano ya kusimamisha mapigano yanatakelezwa.

Urusi na Marekani zina misimamo tofauti kuhusiana na mgogoro huo wa Syria, wakati Urusi ikimuunga mkono Rais wa Syria Bashar al Assad , Marekani kwa upande wake inaunga mkono upande wa upinzani lakini mataifa yote hayo mawili yenye nguvu duniani yamekuwa yakifanya juhudi za kuhakikisha hatua ya kusimamisha mapigano nchini Syria inatakelezeka.

Wakati huohuo, Rais Obama alisisitiza kauli yake hapo jana kuwa Rais Assad anapaswa kuondoka madarakani ili amani ya kudumu iweze kupatikana nchini Syria.

Iran ambayo pia inaunga mkono utawala wa Rais Bashar al Assad tayari imeripotiwa kuondoa baadhi ya wanajeshi wake nchini Syria. Hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa kauli iliyotolewa hapo jana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani,John Kerry.

Uturuki yasisitiza usalama wake kwanza.

Wakati huo huo; Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema Uturuki haitabanwa na hatua hiyo ya kusimamisha mashambulizi iwapo itaamini kuwa usalama wake uko hatarini, na kuongeza kuwa marufuku hiyo ya kutoendelea na mapigano inalenga Syria pekee lakini, kwa upande wake usalama ndani ya taifa lake ni muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote.

Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu
Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet DavutogluPicha: Reuters/G. Garanich

Aidha katika kuelekea utekelezaji wa makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano, Umoja wa Mataifa umetoa taarifa ya kuonyesha matumaini ya usambazaji wa misaada ya kiutu nchini Syria.

Jan Egeland ambaye ni mshauri kwa Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na mgogoro huo wa Syria amesema zaidi ya malori 180 yaliyokuwa yamebeba misaada ya kiutu yamefanikiwa kufika katika maeneo sita yaliyokuwa yamezingirwa katika kipindi cha wiki mbili.

Mwandishi : Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri : Daniel Gakuba