1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron aitembelea Nigeria

Saumu Mwasimba
3 Julai 2018

Ziara hiyo ya kiongozi wa Ufaransa ni mwendelezo wa juhudi zake za hivi karibuni za kutafuta ushirikiano wa karibu na nchi zinazozungumza lugha ya Kiingereza barani Afrika.

https://p.dw.com/p/30kk6
Mauretanien Frankreich Afrikanische Union
Picha: picture-alliance/L.Marin

Miaka 15 baada ya kuhudumu akiwa mwanafunzi katika ubalozi wa Ufaransa mjini Abuja, Macron anarudi tena katika mji mkuu huo wa Nigeria akiwa kama kiongozi wa nchi na anakwenda kukutana na Rais Buhari kabla ya kusafiri kuelekea kusini katika mji wa Lagos.

Rais huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 40 aliyewahi kuwa mfanyakazi wa Benki ya Uwezekaji anayezungumza kwa ufasaha Kiingereza, ameonesha dhamira ya kuimarisha uhusiano na makoloni ya zamani ya Ufaransa lakini pia kuimarisha biashara na nchi za Kiafrika zinazozungumza lugha ya Kiingereza.

Aliwahi kuitembelea Ghana mwaka jana na Nigeria nchi ambayo ina uchumi mkubwa barani Afrika na pia taifa lenye utajiri mkubwa wa mafuta barani humo ndio kituo chake kingine cha kimkakati.

Nigeria, nchi ambayo ina wakaazi zaidi ya milioni 180, inazalisha kiasi mapipa milioni 2 ya mafuta ghafi kwa siku na ni mshirika mkuu wa kiuchumi kwa Ufaransa.

Katika mji wa Abuja, usalama ndio suala linalotegemewa kuwa ajenda kuu kutokana na eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria kuwa kitovu cha harakati za kundi la itikadi kali la Boko Haram kwa miaka tisa, ambalo uasi wake umeenea kote katika eneo linalozunguka Mto Chad.

Nigeria pamoja na majirani zake wanaozungumza Kifaransa kama Cameroon,Chad na Niger wanahusika katika operesheni ya pamoja ya kijeshi kukabiliana na kundi hilo ambalo limeshaua kiasi watu 20,000 mpaka wakati huu.

Kamerun Symbolbild Soldaten im Norden ARCHIV
Picha: Getty Images/AFP/R. Kaze

Wakati huo huo, Nigeria kwa sasa inakabiliwa na kurudi upya kwa vurugu kati ya wafugaji wa kuhamahama na wakulima, ambazo kufikia sasa zimeshasababisha watu 1,000 kuuwawa  tangu mwezi Januari mwaka huu.

Hali hii imemuweka Rais Buhari mwenye umri wa miaka 75, na ambaye aliwahi kuwa mtawala wa kijeshi, kwenye wakati mgumu, huku mwenyewe akitafuta nafasi ya kurudi tena madarakani kwa muhula wa pili uchaguzi utakapoishwa Februari mwaka ujao.

Mkutano wa Rais Macron mjini Lagos utahusiana zaidi na masuala ambayo sio ya kidiplomasia ambapo hasa yatalenga zaidi kwenye kuuangalia mji huo mkubwa wenye shughuli nyingi za kibiashara na mambo ya sanaa na utamaduni unaokaliwa na  wakaazi milioni 20.

Nigeria Angriff von Nomaden im Bundesstaat Plateau | Muhammadu Buhari, Präsident
Picha: Reuters/Nigeria Presidency

Baadaye usiku leo rais huyo wa Ufaransa anatarajiwa kuzindua rasmi msimu wa tamasha la utamaduni wa Kiafrika ambao utafanyika nchini Ufaransa mwaka 2020, hii ikiwa ni shughuli inayotangaza zaidi muziki, fasheni na michezo ya filamu za majukwaani.

Uzinduzi huo nchini Nigeria utafanyika alikotokea mwanamuziki mashuhuri wa Afrobeat, Fela Kuti, mpinzani wa serikali, na hilo limewashangaza Wananigeria wengi.

Hakuna rais yoyote aliyewahi kutembelea rasmi eneo hilo ambako ni nyumbani kwa mtu anayetambulika kama rais wa watu weusi. Ingawa pia kuna Wanigeria ambao hawakushangazwa na hatua hiyo ya rais wa Ufaransa kwa sababu wanafahamu Ufaransa ni nchi ya utamaduni na zaidi Macron ni rais kijana.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef