1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron ataka mageuzi ya Umoja wa Ulaya

5 Machi 2019

Emmanuel Macron ameandika barua ya wazi inayotaka mageuzi mbalimbali katika Umoja wa Ulaya ili kupunguza ushawishi wa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia na kuepuka kile kilichotokea Uingereza iliyoamua kujitenga.

https://p.dw.com/p/3EUS3
Weltmacron (Bodo Zemke)
Picha: DW/B. Zemke

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ameandika barua ya wazi inayotaka mageuzi mbalimbali katika Umoja wa Ulaya, hatua inayolenga kupunguza ushawishi wa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia na wakati huo huo kurejesha madaraka zaidi kwa mataifa wanachama wa Umoja huo ili kuepuka kile kilichotokea Uingereza iliyoamua kujitenga. 

Barua hiyo ya wazi ya Rais Macron imeandikwa miezi mitatu kabla ya uchaguzi wa bunge la Ulaya kufanyika na imechapishwa na magazeti yapatayo 28 katika bara lote la Ulaya siku ya Jumanne.

Pamoja na mengine, mapendekezo hayo yanazingatia uundwaji wa taasisi ya kulinda demokrasia barani Ulaya, ambayo itakua inasaidia kuzikinga nchi za Umoja wa Ulaya dhid ya mashambulizi ya mtandaoni na kuingiliwa katika chaguzi zao. Aliongeza kuwa kuchangiwa hela kwa vyama vya siasa na madola makubwa ya nje inabidi pia kupigwe marufuku.

Frankreich Rede Emmanuel Macron - Antisemitismus in Frankreich
Picha: picture-alliance/dpa/AP/L. Marin

Macron ameshauri kuundwa kwa chombo cha pamoja cha ulinzi wa mipaka na sera moja ya wakimbizi. Ameshauri pia kutengenezwa mkataba mpya ambao utaainisha shughuli za Umoja wa Ulaya kwenye upande wa kujilinda na jinsi Umoja huo utakavyohusiana na Jumuiya ya Kujiami ya NATO na marafiki zao wengine wa Ulaya na kuongeza michango ya jeshi hilo la NATO.

Kwenye upande wa uchumi, Macron anataka mabadiliko katika sera ya ushindani ambazo zitadhibiti biashara ambazo zitaenda tofauti na maslahi ya Ulaya kwenye upande wa kuzingatia kutunza mazingira, kulinda data za watu na kulipia kodi zao ipasavyo. Kwenye upande wa mazingira ameshauri kundwa kwa Benki ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Ulaya na kikosi kwa ajili ya usalama wa chakula barani ulaya.

Ingawa kuna mapendekezo hayo inategemewa kutakua na upinzani mkubwa kutoka kwa waziri mkuu wa Hungary, Viktor Orban, ambaye hivi karibuni alitoa bango katika kampeni zake kumtuhumu mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker, kwamba anasaidia kupelekea kwa uhamiaji haramu barani humo. Pia Ufaransa imekua kwenye ugomvi na nchi jirani mfano Italia baada ya Ufaransa kumwita nyumbani balozi wake wa Italia kwa kisa cha makamu wa waziri mkuu wa Italia kukutana na waandamanji wa vizibao vya njano waopinga sera za Macron. Pia hivi karibuni Ufaransa ilitofautiana na Ujerumani kwenye upande wa uuzaji wa silaha na bomba la gesi la Nord Stream 2 linalotegemewa kuleta gesi kutoka Urusi kuja Ulaya.

Mwandishi: Harrison Mwilima/DPA

Mhariri: Mohammed Khelef