1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron atoa mapendekezo ya mageuzi EU

Amina Abubakar26 Septemba 2017

Macron amependekeza Umoja wa Ulaya uwe na bajeti ya pamoja ya Ulinzi, kikosi cha pamoja cha kijeshi, na kikosi cha polisi wa mipakani kiundwe ili kuhakikisha kunakuwepo na mipaka inayolindwa vizuri.

https://p.dw.com/p/2klFW
Emmanuel Macron Rede Paris
Picha: Reuters/L.Marin

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameweka wazi mapendekezo yake kuelekea mageuzi ya Umoja wa Ulaya, kwa kutaka kuuendeleza ukanda unaotumia sarafu moja ya Euro na kutoa mawazo ya ushirikiano zaidi wa ulinzi na uhamiaji. 

Rais Macron alikuwa anaainisha vipaumbele vyaka kabla ya Kansela wa Ujerumani kuanza kazi ngumu ya kuunda serikali ya muungano baada ya chama chake kupata pigo katika uchaguzi uliyomalizika siku ya Jumapili, jambo ambalo linaweza kuzuwia uwezo wake wa kumsaidia macro kufanikisha ajenda yake ya mabadiliko ndani ya Umoja wa Ulaya. 

Katika hotuba yake aliyoitoa katika chuo kikuu cha Sorbonne mjini Paris, rais huyo wa Ufaransa amesema Umoja wa Ulaya unapaswa kuwa na bajeti ya pamoja ya Ulinzi na kupendekeza kikosi cha pamoja cha kijeshi, huku akitaka uundwaji wa kikosi cha polisi wa mipakani ili kuhakikisha kunakuwepo na mipaka inayolindwa vizuri.

Kikosi cha pamoja cha Ulaya

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/L. Marin

Ulaya inapaswa kuwa na kikosi cha pamoja kama ilivyo kwa muungano wa NATO na inahitaji kuwa na mkakati wa pamoja. Macro ameendelea kusema kwamba ifikapo mwaka wa 2020 kikosi hicho cha pamoja cha kuingilia kati cha Umoja wa Ulaya kinapaswa kuwa tayari pamoja na kituo cha ujasusi cha Ulaya.

Rais Macron amesema Ulaya inayoyumba kwa sasa inaonyesha athari za utandawazi, na njia pekee inayohakikisha siku za usoni za Umoja huo ni kujenga tena kanda huru, iliyo na umoja na demokrasia.

"Mwanzoni mwa mwaka mmoja unaokuja Ulaya inapaswa kuwa na kikosi cha pamoja cha kuingilia kati, bajeti ya pamoja na ulinzi na kikosi cha pamoja cha mafundisho," amasema Macron na kuongeza kuwa, Umoja wa Ulaya unapokuwa imara ndiyo hatua za kulinda mipaka zitakapoimarika na kukaribisha wale wanaotaka ulinzi kwa njia ya heshima na wakati huo huo kuwarejesha nyumbani wale ambao hawatakuwa na mahitaji ya kupata hifadhi.

Afrika kama kitisho au mshirika?

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/F. Bensch

Amesema haiwezi tena kuiangalia Afrika kama kitisho lakini kama mshirika kwa hiyo fedha zamaendeleo ni lazime ziongezwe katika kanda hiyo.

Macron aliingia madarakani mwezi May mwaka huu akiahidi kuliimarisha eneo linalotumia sarafu ya euro na kuongeza muingiliano wa Umoja wa Ulaya huku Umoja huo ukijitayarisha kuiaga Uingereza. Macron ana shauku ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuidhinisha ajenda yake ya mageuzi inayojumuisha mpango wa kuyapa mataifa 19 wanachama wa Umoja wa Ulaya Waziri wa fedha bajeti na bunge.

Kwa sasa Angela Merkel anatarajiwa kujaribu kuunda serikali itakayowajumuisha Free Democratic (FDP), ambaye kiongozi wake ni mkosoaji wa wazi wa ajenda za Umoja wa Ulaya za rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.  Lakini licha ya hayo Macron ametumia hotuba yake kushinikiza mabadiliko  ya taasisi, mipango ya kukuza Umoja wa Ulaya na miradi mipya katika sekta ya teknolojia, ulinzi na nishati.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP/DPA

Mhariri: Iddi Ssessanga