1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madagascar inafanya uchaguzi wa wabunge leo

Angela Mdungu
27 Mei 2019

Madagascar inafanya uchaguzi wa wabunge hii leo kukiwa na mchuano mkali kati ya Rais Andry Rajoelina na mpinzani wake Marc Ravalomanana

https://p.dw.com/p/3JB4s
Wahlen Madagaskar Stimmabgabe
Picha: picture-alliance/dpa

Mchuano huo ni baada ya kushindwa kwa Ravalomanana katika uchaguzi uliopita ambaye sasa amekuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono wagombea wa chama chake cha TIM na akiwa  amedhamiria kushinda kile anachokiita awamu ya tatu ya mchuano kati yake na Rais Rajoelina.

Rais Rajoelina na mpinzani wake Ravalomanana wamekuwa wakizitawala siasa za Madagascar tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, wakati mwingine wakishirikiana lakini zaidi wakipambana ili kupata madaraka zaidi. Wakati akihutubia mwanzoni mwa kampeni za bunge, Ravalomanana aliwaambia wafuasi wake kuwa hawakufurahishwa sana na matokeo ya kiti cha Urais, lakini hawana budi kuwa thabiti kwani wao ni washindi.

Hata hivyo Rais Rajoelina amekuwa akijibu hayo bila ajizi, akifanya uzinduzi wa miradi nchini kote ili kufikisha ujumbe wake. Wiki iliyopita, alituma ujumbe kupitia ukurasa wake wa Tweeter na kusema, chama chake kimedhamiria kufanya kazi ili kubadilisha maisha ya raia wa Madagascar. Kuta za mji mkuu wa nchi hiyo, Antananarivo zimetawaliwa na mabango ya uchaguzi, wakati misafara ya magari yenye vipaza sauti ikipita  na vipeperushi kwa ajili ya wafuasi pamoja na fulana zenye picha za wagombea na kuufanya mji kuchangamka.

Kura zinapigwa nchini humo baada ya  machafuko yaliyosababisha Rajoelina na Ravalomanana kuweka kando tofauti zao mwaka uliopitaili kupinga sheria mpya za uchaguzi zilizowekwa hapo awali na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hery Rajaonarimampianina. Baada ya miezi miwili ya maandamano mitaani, serikali ilianguka na Rajaonarimampianina akaachwa mbali kwenye nafasi ya tatu katika nafasi ya Urais.

Madagaskar Wahlen - Wahlsieger und neuer Präsident Andry Rajoelina
Rais wa Madagascar Andry RajoelinaPicha: Getty Images/AFP/Rijasolo

Mmoja wa wagombea wa chama cha TIM cha Ravalomanana, Feno Ralambomanana amesema, alisikitika baada ya mgombea wa chama chake kushindwa lakini hatua hiyo imewapa motisha kutafuta ushindi wa viti vingi katika uchaguzi wa bunge ili kuhakikisha kuna utulivu na kuepuka machafuko ya kisiasa, katika miaka ijayo.

Hali ya wasiwasi juu ya utulivu yatanda

Hata hivyo hakuna uhakika kwamba kura inayopigwa  jumatatu italeta utulivu ambao pande zote zinasema  zinauhitaji, wakati wagombea 800 wakiwania viti 151 vya bunge, 500 kati ya hao wakiwa ni wagombea binafsi. Mchambuzi wa kisiasa Tohavina Ralambomahay ameliambia shirika la habari la AFP kuwa katika uchaguzi huo, uwezekano wa wagombea binafsi kushinda viti vingi, kwani wapiga kura wengi wanataka kuzivunja kambi za mahasimu wawili; kambi za Rajoelina na Ravalomanana.

Hat hivyo dakika za mwisho za kampeni hizo uchaguzi wa wabunge zilitawaliwa na tuhuma za ufisadi dhidi ya zaidi ya nusu ya wasadizi wanaoondoka kwenye nafasi zao. Tume ya kupambana na rushwa, iliwakabidhi waendesha mashitaka orodha ya watuhumiwa 79, ambao wote wanatuhumiwa kukubali rushwa yenye thamani ya dola 14,000 ili wapige kura kuunga mkono sheria za uchaguzi za Rajaonarimampianina.Rajoelina na Ravalomanana wote wamewaahidi wapiga kura kuwa watahakikisha wanatokomeza mambo kama hayo.

 Kwa mujibu wa benki ya dunia, Madagascar, ambayo ni koloni la zamani la Ufaransa ni maarufu zaidi kwa uzalishaji wake wa vanila lakini bado ni moja kati ya mataifa masikini zaidi duniani huku asilimia 76 ya raia wake wakiishi katika umasikini. Kisiwa hicho ambacho pia kinafahamika kwa kuwa na  wanyamapori wa kipekee kinategemea zaidi misaada ya kigeni na kina historia ndefu ya machafuko na mapinduzi ya kijeshi.