1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madini ya DRC yaendelea kuporwa

2 Februari 2011

Majeshi ya serikali na yale ya waasi mashariki mwa DRC yanatuhumiwa kutumia mwanya wa utulivu kuendelea kupora maili asili hususan madini yakiwemo dhahabu na madini mengine yenye dhamani ya dola billioni 1.3 kila mwaka.

https://p.dw.com/p/108tl
Wanajeshi wa serikali ya DRCPicha: AP

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika moja lisililo la kiserikali lenye makao yake mjini Washington Marekani liitwalo Enough Project.

Shirika hilo limesema jeshi la DRC, waasi wa FDLR pamoja na wanamgambo wa Mai Mai Cheka wamekuwa wakichimba na kuchukua madini hayo kwenye majimbo ya Kivu ya Kaskazini na Kusini pamoja na Jimbo la Maniema.

Waasi wa Mai Mai Cheka pamoja na makundi mengine ya waasi, wanahusika na vitendo vya ubakaji wa wanawake kiasi ya 300 vilivyofanyika mwaka jana katika maeneo ya Kalikale huko Kivu Kaskazini.

Uchunguzi uliyofanywa na shirika hilo la Enough Project umebainisha kuwa wakati kunapokuwa na amani, makundi hayo yanaungana na kuchimba madini hayo ambayo mbali ya dhahabu ni yale yanayotumika katika utengenezaji wa simu za mkononi na vifaa vingine vya elektroniki.

Mwanzilishi mwenza wa shirika hilo John Prendergast amelitaka Bunge la Marekani pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuchukua hatua mujarabu kukabiliana na biashara hiyo haramu huko Mashariki mwa Kongo, hatua ambazo ni pamoja na kuzuia ununuaji wa madini hayo.

Serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imepitisha sheria inayozuia shughuli za madini kwenye eneo hilo, lakini hata hivyo hakuna utekelezaji wa sheria hiyo.

Prendergast amesema ni muhimu kwa Marekani kuongoza juhudi za kuwekwa kwa udhibiti wa kimataifa katika biashara ya madini yanayotoka eneo hilo la Mashahriki mwa Kongo, ili kuyazuia makundi yenye silaha kufaidika na madini hayo.

Baraza la Kongress la Marekani mwaka jana lilipitisha sheria inayotaka makampuni kuelezea matumizi yao ya madini kutoko Kongo.

Amesema fedha ambazo makundi hayo yamekuwa yakipata kutokana na biashara hayo zimechangia kuwepo kwa mapigano pamoja na vitendo vya uovu wanavyofanyiwa raia wa eneo hilo na kwamba wanaendesha biashara hiyo katika mtindo wa mafia.

´´Kimsingi makundi yenye silaha mashariki mwa kongo yanafanya shughuli zao kama ilivyo kwa kundi la mafia.Migodi yenye ya madini inadhibitiwa na makundi hayo ya wanamgambo na yamekuwa yakipeleka madini hayo kimagendo katika nchi jirani za Uganda na Rwanda.Vituo hivyo vya kupitishia biashara hiyo pia vinadhibitiwa na makundi hayo.Kwa hiyo maeneo hayo yote yanatengeneza kiwnago kikubwa cha fedha kwa kutoza ushuru, kupora madini hayo na kuyauza kimagendo nje ya nchi´´amesema Pendergast.

Ikumbukwe ya kwamba katika uchunguzi wake kwenye eneo hilo la Mashariki mwa Kongo, Umoja wa Mataifa, uliwanyooshea kidole maafisa wa jeshi la Kongo pamoja na wale wa kundi la zamani la waasi lililokuwa likiungwa mkono na Rwanda la CNDP, kujihusisha na biashara hiyo haramu.

Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inakadiria kuwa madini yenye thamani ya kiasi cha dola billioni 1.3 yamekuwa yakiunzwa nje ya nchi hiyo kimagendo kila mwaka.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA

Mpitiaji:Oummilkheir