1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maduro adokeza juu ya mikutano ya siri na mjumbe wa Marekani

Zainab Aziz
15 Februari 2019

Mwezi mmoja tangu Venezuela ilipotumbukia kwenye mgogoro wa kisiasa, Rais Nicolas Maduro ameliambia shirika la habari la AP kwamba serikali yake imefanya mazungumzo ya siri na utawala wa Marekani.

https://p.dw.com/p/3DTTN
USA UN New York l Venezuelanischer Außenminister Jorge Arreaza zur Krise in Venezuela - begleitet von Diplomaten aus 16 Ländern
Picha: picture-alliance/Xinhua/L. Muzi

Maduro ameukosoa ushari wa Rais Donald Trump wa Marekani na msimamo wake dhidi ya serikali yake ya kisoshalisti. Rais huyo wa Venezuela amesema Maduro alisema haondoi matumaini ya kukutana na rais wa Marekani ili kutafuta njia za kuutatua mgogoro uliotokana na nchi hiyo kumtambua kiongozi wa upinzani Juan Guaido kama rais wa mpito wa Venezuela aliye na haki ya kuliongoza taifa hilo.

Rais Maduro amefahamisha kuwa wakati wa mikutano miwili ya mjini New York, waziri wake wa mambo ya nje alimwalika mjumbe maalumu wa Marekani anayeshughulikia mgogoro wa Venezuela, Elliott Abrams, kuitembelea Venezueala kwa faragha, au wazi bila kificho.

Maduro amesema yuko tayari kukutana na mjumbe huyo wakati wowote na mahala popote ingawa Rais huyo wa Venezuela hakutoa maelezo zaidi juu ya mikutano ya mjini New York kati ya waziri wake wa mambo ya nje na mjumbe maalumu wa Marekani iliyofanyika kwa saa kadhaa.

Afisa mmoja mkuu kwenye utawala wa Marekani ambaye hana mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari sema kwa hadharani amesema kwamba maafisa wa Marekani wako tayari kukutana na maafisa wa serikali ya Venezuela, ikiwa ni pamoja na Maduro mwenyewe, kujadili mipango ya kuondoka kwao madarakani.

Venezuela inakabiliwa na machafuko ya kisiasa yaliyotokana na wito wa Marekani wa kumtaka Rais Maduro ajiuzulu miezi miwili baada kufanyika uchaguzi wa urais ambapo Maduro alishinda muhula wake wa pili hatua ambayo Marekani na washirika wake wa Amerika ya Kusini wanasema ushindi huo sio halali. Mpinzani wake, Juan Guaido mwenye umri wa miaka 35, ameongeza changamoto za kisiasa nchini Venezuela baada ya kuhoji uhalali wa Maduro kuendelea kuwepo madarakani.

Waziri wa mambo ya nje wa Venezuela Jorge Arreaza
Waziri wa mambo ya nje wa Venezuela Jorge ArreazaPicha: picture alliance/dpa/AP/B. Matthews

Urusi na China zilijiunga na Cuba, Iran, Korea ya Kaskazini na nchi nyingine kadhaa katika Umoja wa Mataifa mnamo siku ya Alhamisi kumuunga mkono Rais wa Venezuela Nicolas Maduro katika mvutano wake na Marekani. 

Waziri wa Mambo ya nje wa Venezuela Jorge Arreaza aliwaambia waandishi wa habari kundi hilo litachukua hatua katika siku zijazo kuuelezea ulimwengu juu ya hatari ambazo zinawakabili watu wa  Venezuela kwa sasa.Arreaza amesema sote tuna haki ya kuishi bila kitisho cha matumizi ya nguvu na bila ya hatua zilizo kinyume cha sheria zisizo halali. Arreaza alikuwa na wanadiplomasia kutoka Urusi, China, Iran, Cuba, Nicaragua, Bolivia, Korea ya Kaskazini, Syria, mwakilishi wa mamlaka ya Palestina na wanadiplomasia kutoka nchi za Karibik alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Wanadiplomasia hao wamesema takriban nchi 50 zimejiunga na kundi hilo ili kuisaidia serikali ya Maduro. Mataifa 193 wanachama wa Umoja wa wamegawanyika kati ya nchi zinazomuunga mkono kiongozi wa upinzani Juan Guaido, ambaye alijitangaza kuwa rais wa mpito mnamo Januari 23, na wale ambao wanamuunga mkono Rais Maduro.

Wakati huo huo  bilionea wa Uingereza Richard Branson anaandaa tamasha kubwa kwa ajili ya kuchangisha kiasi cha dola milioni 100 zitakazotumiaka kwa ajili ya kuwasaida watu wa Venezuela na harakati za kumshinikiza Maduro ajiuzulu.

Tamasha hilo litafanyika Februari 22 katika mji wa Cucuta nchini Colombia ulioko kwenye mpaka na Venezuela ambalo litaonyeshwa moja kwa moja kwenye mtandao wa Intaneti.

Mwandishi:Zainab Aziz/APE/AFPE

Mhariri: Josephat Charo