1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walionekana wakiimba, ´Amka Ulaya`

Admin.WagnerD7 Desemba 2017

Maelfu ya waandamanaji raia wa Catalonia, wamejikusanya katika mji wa Brussels Ubelgiji, leo ili kuonyesha mshikamano wao  kwa rais wa Catalonya, Carles Puigdemont aliyeondolewa madarakani.

https://p.dw.com/p/2ox6j
Brüssel Demonstration für unabhängiges Katalonien
Picha: Reuters/Y. Herman

Walionekana wakiimba, ``Amka ulaya`` huku wakipeperusha, bendera ya Waestelada waliojitenga, yenye rangi, nyekundu, njano na buluu. Waandamanaji hao walikusanyika katika eneo lililo karibu na makao makuu ya Umoja wa Ulaya, kabla ya kuandamana kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo.

``Hatuwezi kumtelekeza rais wetu ambaye yupo uhamishoni hapa`` hayo ni maneno ya Antoni Lienad, mmoja waandamanaji aliyeonekana amevaa bendera  mabegani mwake.

``Tupo hapa kuendelea na harakati kwa ajili ya uhuru wetu na kutaka uhuru wetu na wa wafungwa wetu wa kisiasa.``

Polisi wa mjini Brussels  walikuwepo, lakini maandamano ya awali yalionekana kutawaliwa na amani. Wengine walionekana wamebeba mabango yanayoukosoa Umoja wa Ulaya kwa kutoishinikiza Madrid. Bango mojawapo lilionyesha sura ya Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, ikiwa na neno ´Demokrasia´, likiwa na alama ya kuuliza.

Watoto na watu wana familia wengine, ni miongoni mwa walioshiriki katika maandamao hayo wakiwa na matumiani makubwa, licha ya baridi kali na mvua.

Timmermans asema hakuna mabadiliko kwenye Tume ya Ulaya

Umbali mdogo kutoka yalipo makao makuu ya Umoja wa Ulaya, msaidizi wa Juncker, Frans Timmermans, aliwaambia wanahabari kuwa ameyapokea  bila kinyongo mazingira chanya ya maandamano hayo, ambayo yamefanyika wakati kampeni za uchaguzi wa Catalonya, zimeanza.

Hata hivyo, Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje, wa Uholanzi, alisema hakuna mabadiliko katika sera ya tume hiyo,  kwamba malumbano na mamlaka za Barcelona, ambao wameondolewa madarakani, bado linabaki jambo la ndani, ambalo Umoja wa Ulaya  hauna haja ya kuingilia. Alisema  demokrasia ya Uhispania, inafanya kazi kwa kufuata maadili ya Umoja wa Ulaya.

Puigdemont na mawaziri wanne wa zamani, walikimbilia Brussels, Novemba mwaka huu wakidai kuwa wanataka kulipeleka suala hilo katika kiwango cha Ulaya, baada ya Uhispania, kuwashitaki kwa makosa ya uchochezi na uasi,   wakati wa kura ya maoni kuhusu uhuru wa Catalonya, Oktoba mwaka huu.

Brüssel Demonstration für unabhängiges Katalonien
Picha: Reuters/Y. Herman

Nil Monso, ni miongoni mwa waandamanaji hao, na alisema wafungwa wote wa kisiasa ni vyema waakachiwa huru.

``Nafikiri haitoshi kuwaachia watu wachache, lazima wawaachie wote. Huwezi kuwashutumu baadhi ya wanasiasa wa serikali yetu kwa kupiga kura, hiyo ni demokrasia. Suala la kupiga kura, wakati wote linatakiwa liwe juu ya sheria, ``alisema

Serikali kuu ya Uhipsnia mjini Madrid iliondoa amri ya kukamatwa kwa viongozi hao watano na nchi za  Ulaya , Jumatatu wiki hii, lakini Pugdemont akasema ataendelea kubaki, kwani bado wanaweza kukamatwa Uhispania iwapo watarudi nchini humo katika uchaguzi wa majimbo, utakaofanyika Catalonya, Desemba 21.

Waandaaji wa maandamano hayo wanakadiria kuwa, watu 20,000 watahudhuria maandamano hayo, leo huku kukiwa na tetesi kuwa Puigdemont mwenyewe, atahutubia.

 Waandamanaji walifika wakiwa katika mabasi na  magari yaliyoundwa na  vitanda vya kulalia yenye namba za usajili  za Uhispania. Walianza kwa kukusanyika katika eneo la wazi la Cinquantenaire, Brussel saa chache kabla ya kuanza kwa maandamano hayo.

Maandamano hayo, yataelekea makao makuu ya Tume ya Ulaya na kuishia katika mnara ulio kati ya baraza la Ulaya na Bunge la Ulaya. Hizo ni taasisi kuu tatu za Umoja wa Ulaya.

Ulaya, kwa kiasi kikubwa inaiunga mkono serikali ya Uhispania, kuhusu suala la Catalonya, ikisema kuwa, ni suala la ndani la Uhispania.

 Mwandishi: Florence Majani(AFP; Reuters)

Mhariri: Saumu Yusuf