1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maendeleo katika Ulimwengu wa Kiarabu

11 Agosti 2009

Nchi za Kiarabu zinakabiliwa na mizozo ya kisiasa na kiuchumi, uvamizi kutoka nje,kasoro katika elimu na kulinganishwa na mataifa mengine, idadi ya vijana wasio na ajira katika nchi hizo ni kubwa sana.

https://p.dw.com/p/J7pq

Hayo ni baadhi ya matokeo ya utafiti yaliyoelezwa na Umoja wa Mataifa katika "Ripoti juu ya Nchi za Kiarabu ya Maendeleo ya Binadamu 2009". Mtu anapaswa kuipekua sana ripoti hiyo kabla ya kuona kile kilicho kizuri kwa mfano, uchafuzi wa mazingira katika nchi za Kiarabu ni wa kiwango cha chini kabisa kote duniani. Lakini mtu akidhani kuwa hiyo ni kwa sababu ya sera bora za mazingira au magari yaliyojaa katika miji mikubwa ya Kiarabu ni yale yanyotoa gesi zinazochafua kidogo mazingira, basi anakosea. Tarakimu za wastani kweli zinaonyesha kuwa hewa ni safi katika nchi za Kiarabu. Lakini hali hiyo ingeweza pia kuwa vingine kwani kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa vipimo hivyo vya usafi ni matokeo ya kutokuwepo viwanda vingi katika nchi hizo za Kiarabu.

Na hicho ni kiini cha ripoti mpya ya maendeleo: yaani uhaba, kwani katika nchi za Kiarabu kuna kasoro nyingi mno. Si upungufu wa viwanda tu bali kunakosekana pia mfumo wa afya unaofanya kazi, maji safi ya kunywa na hasa kuna uhaba wa demokrasia, utawala bora na hata haki za binadamu na heshima kwa wananchi wake wenyewe.

Inasikitisha kuwa katika ulimwengu wa Kiarabu,licha ya mabadiliko fulani yaliyotia moyo miaka hii ya karibuni bado hakuna hata serikali moja hii leo isiyoweza kuelezwa kama ni utawala wa mabavu. Miongoni mwao, ni Libya na Syria na utawala wa kifalme katika nchi za Ghuba na hata nchi zenye uhuru fulani na kupenda kuonekana kama nchi yenye demokrasia kama vile Misri. Katika ulimwengu wa Kiarabu,Misri ni mshirika wa dhati wa magharibi na inaongoza katika jitahada za kupatana na Israel lakini vile vile, ni nchi inayofumbia macho vitendo vya mateso vinavyotokea katika vituo vya polisi na kisiasa haizingatii matakwa ya wananchi wake.

Ni dhahiri kuwa sababu za matatizo ya maendeleo katika ulimwengu wa Kiarabu zinaweza kupatiwa ufumbuzi huko huko. Kinachohitajiwa ni upeo, mawazo mapya na jitahada mpya, hasa katika sekta ya elimu,kwani hapo ndipo kwenye dosari kubwa na kasoro hiyo, inazuia kuleta maendeleo endelevu katika jamii. Lakini serikali nyingi hushughulikia zaidi maslahi ya kubakia madarakani. Hata hivyo,nchi za magharibi hazina budi kushirikiana na serikali hizo lakini wakati huo huo zinapaswa pia kushughulikia zaidi jamii za kiraia.

Ikiwa nchi za Kiarabu zenyewe hazitosuluhisha mizozo yake na idadi ya wakazi katika nchi hizo nyingi, ikiendelea kuongezeka kama ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na hamu ya kuhamia nchi za kigeni ikizidi kuwa kubwa huku ikiwepo hatari kwa kizazi kijacho kuwa na misimamo mikali, basi hayo yote, hayawezi kupuuzwa hasa na Umoja wa Ulaya. Kwani yote hayo yanaweza kusababisha hatari karibu na mipaka yake.

Mwandishi: R.Sollich/ZPR

Mhariri:M.Abdul-Rahman