1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko Burkina Faso

Oumilkher Hamidou3 Septemba 2009

Mvua za masika zaathiri maisha na mimea Afrika magharibi

https://p.dw.com/p/JOHz
Watu wanasalimisha maisha yao baada ya mafurikoPicha: picture-alliance/dpa

Watu watano wamepoteza maisha yao kufuatia mafuriko katika mji mkuu wa Burkina Faso-Ouagadougou,vitongoji vyake na miji mengine ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kali iliyokua ikinyesha katika eneo hilo la Afrika magharibi.

Katika nchi jirani ya Niger,watu wasiopungua wawili wamepoteza maisha yao na 20 elfu kuvunjikiwa na nyumba zao kwasababu ya mvua hizo zilizosababisha mafuriko makubwa pia nchini Senegal.

Nchini Burkina Faso serikali ilikutana kwa dharura jana kuzungumzia hatua zinazobidi kuchukuliwa.Akizungumza na waandishi habari,waziri mkuu Tertius Zongo amesema mwishoni mwa mkutano huo,"miili ya watu watatu imeokolewa mjini Ougadougou,bibi mmoja ameuwawa Kiembera,umbali wa kilomita 225 toka mji mkuu huo na mtu mwengine amekufa baada ya kuangukiwa na nyumba."

Kwa mujibu wa serikali,daraja tatu hazipitiki mjini Ougadougou.

Sehemu kubwa ya hospitali kuu ya Yalgado Ouédraogo imefunikwa na maji,sawa na kinu cha umeme cha mji huo.

Zaidi ya hayo mafuriko hayo katika nchi hiyo mashuhuri kwa maonyesho ya filamu barani Afrika-FESPACO, yameangamiza sehemu ya filamu 1500 zilizokua zikihifadhiwa katika makao makuu ya maonyesho hayo .

Majumba kadhaa yameporomoka katika vitongoji vya mji mkuu ambako wakaazi wamekua wakijaribu kusalimisha chochote walichoweza kukipata toka magofu ya nyumba zao.

Kwa mujibu wa waziri mkuu Tertius Zongo,watu laki moja na nusu wamevunjikiwa na nyumba zao na wanahitaji kusaidiwa.Hadi sasa watu laki moja na elfu kumi wamehamishiwa katika vituo vya muda ikiwa ni pamoja na shule na wengine wameamua kuhamia kwa majirani zao.

Wanaharakati wa mashirika ya misaada ya Burkina Faso,nchi hiyo ndogo yenye wakaazi milioni moja,wanasema wanashindwa kufanya kazi yao ipasavyo kutokana na kuvunjika daraka na njia hazipitiki.

Blaise Compaoré Präsident Burkina Faso
Rais Blaise Compaore wa Burkina FasoPicha: picture-alliance/ dpa

Rais Blaise Compaore,anaeitawala Burkina Faso tangu miaka 21 iliyopita ameitaka serikali yake ipitishe hatua za aina pekee kuhakikisha makaazi ya maana mijini.Rais Compaore amesema hayo akiwa mjini Tripoli ambako alihudhuria mkutano wa dharura wa kilele wa Umoja wa Afrika na sherehe za kuadhimisha miaka 40 tangu Muammar Gaddafi aliponyakua madaraka nchini Libya.

Mvua za masika zinazoanza June katika eneo la Afrika magharibi zinasababisha mafuriko makubwa na matope katika eneo hilo.Mnamo mwaka 2007,watu 300 walipoteza maisha yao , zaidi ya laki nane walivunjikiwa na maskani yao na mimea kuangamia.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/AFP/Reuters

Mhariri:M.Abdul-Rahman