1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yaathiri miji kadha nchini Australia

Sekione Kitojo3 Januari 2011

Jeshi la Australia limepeleka misaada ya chakula na madawa kwa watu walioathirika na mafuriko katika mji wa kaskazini mwa nchi hiyo wa Rockhampton.

https://p.dw.com/p/zt6z
Sehemu ya mji wa Rockhampton uliokubwa na mafuriko nchini Australia.Picha: picture alliance / dpa

Jeshi  la  Australia   leo  limepeleka  chakula  na  mahitaji  mengine kwa   watu  walioathirika  na  mafuriko  katika  mji  wa  kaskazini  wa Rockhampton  kabla  haujatengwa  kabisa  na   sehemu  nyingine  za nchi  hiyo , kutokana  na  kuongezeka  kwa  kiwango  cha  maji katika  janga  la  mafuriko  ambapo  watu  kumi  wamefariki.

Watu  wapatao  200,000  wanakadiriwa   kuwa  wameathirika  na mafuriko  makubwa   ambayo  yamefunika  karibu   miji   midogo   22 katika  eneo  la  kaskazini  la  Australia, katika  eneo  ambalo  ni sawa  na  ukubwa  wa   nchi  za  Ujermani  na  Ufaransa. Jeshi limekuwa  likipeleka  chakula  na  madawa  katika  mji  wa Rockhampton ,  wenye  wakaazi  wapatao  75,000,  wakati  mji  huo ulioko  katika  eneo  la  pwani  ukijiweka  tayari  kwa  mafuriko ambayo  yanatarajiwa   kuyatenga  maeneo  kadha  na  sehemu nyingine  za  mji  huo.

Mji  wa  Rockhampton  unaonekana   kama  uko  katikati  ya  bahari, waziri  mkuu  wa  jimbo  la  Qeensland,  Anna  Bligh,  amesema baada  ya  kuangalia  maafa   hayo  akiwa  katika  ndege. Kiasi  cha maji  kinachoelekea  katika  mji  huo  katika  mito  inayopitia  karibu na  mji  huo  kinashangaza.

Uwanja  wa  ndege  umefungwa  wakati   mafuriko  yamezuwia mawasiliano  ya  barabara   upande  wa  kusini  na  magharibi, na kusababisha  wasi  wasi  miongoni  mwa  maafisa   kuwa  eneo  hilo lenye  watu  wengi  huenda  likapungukiwa  na  chakula.

Julia Gillard
Waziri mkuu wa Australia Julia Gillard.Picha: AP

Waziri  mkuu  Julia  Gillard  ametoa  fedha  za  dharura  kwa maeneo  yaliyoathirika  na  mafuriko, ikiwa  ni  pamoja  na  wakulima ambao  wamekuwa  wakikabiliwa  kwa  muda  mrefu  na   ukame, pamoja  na  wafanyabiashara  wadogo  wadogo.

Wakati  mafuriko  yatakapomalizika , tutaona   madhara  makubwa zaidi,  lakini  tutakuwa  tunashirikiana    na  serikali  ya  jimbo  hilo, kujenga  upya  miundo  mbinu  ya  kijamii, Gillard  amewaambia waandishi  habari  mjini  Sydney.

Waziri  mkuu  Gillard  ambaye  alikagua  maeneo  ambayo yameathirika  zaidi siku  ya  Ijumaa, amesema   kuwa katika  baadhi ya  maeneo  haya  yamekuwa  mafuriko  makubwa  kabisa  ambayo hayajawahi  kuonekana, na  kutoa  tahadhari  kwamba  kuna  hatari zaidi  kutokana  na  maji  yanayokwenda  kwa  kasi. Mkurugenzi  wa shirika  la  msalaba  mwekundi  katika  jimbo  la  Queensland,  Greg Goebel,  amesema  shirika  lake  limejiandaa  kwa  hali  hiyo.

"

Tuna  nafasi  ya  watu 1,200, lakini  hatutarajii  kuwa  idadi  itakuwa juu  sana, lakini  tusisahau  kuwa maji  bado  hayajafikia  kiwango cha  juu  kabisa. Maji  katika  mji  huu  yanapanda  kuelekea  katika vituo  vya  uokozi  tulivyoviweka  na  maji  yanaelekea pia  katika maeneo  mengine , kwa  hiyo  watu  wengi  zaidi watakuja  katika maeneo  ya  uokozi.

"

Polisi  wamethibitisha   kufariki  kwa  mtu  wa  tatu  tangu  mafuriko hayo  kutangazwa  kuwa  ni  maafa, ambapo  mtu  mmoja  alifariki baada  ya  gari  lake  kuchukuliwa  na  maji  katika  mto  uliofurika. Watu  kumi  wamefariki  hadi  sasa  tangu  Novemba  30, ikiwa  ni pamoja  na  magari  matatu  ambayo  yamechukuliwa  na  maji.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Othman  Miraj